Thursday, June 28, 2007

FRIJI ISIYOTUMIA UMEME

Hii ni habari njema.Habari hii nimeipata kutoka idhaa ya kiswahili BBC.Ni teknolojia itakayotuwezesha kutumia vyombo vya kupoozea kama vile friji bila ya kutumia umeme.Kilichonivutia zaidi, teknolojia hii ilikuwa ikiongelewa na mtanzania mwenzetu aliyefanya utafiti wake nchini Uingereza.Mwandishi wa habari wa BBC alipomuuliza mhandisi huyu,tarehe 13th March 2007, kuwa kwa nini akiwa kama mwafrika asiisaidie nchi yake kuileta teknolojia hii.

Anamjibu,

“Endapo viongozi wetu na watunga sera watataka kupata utaalamu wangu ili uinufaishe nchi yetu niko tayari”

Swali ninalojiuliza ni kwamba, ni kwa nini hawa tuliowapa dhmana ya kutuongoza hawana mikakati madhubuti na endelevu ya kuwatumia wataalamu wetu walioko ughaibuni hata waliopo nyumbani kwa manufa ya nchi yetu?

Je ni ubutu wa fikra?

Je ni kutokujua?

Au ni nini hasa?

Kuongoza ni kuonyesha njia. Kila mmoja atimize wajibu wake

Wednesday, June 27, 2007

BURIANI AMINA

Ni asubuhi, naamka na ninaingia mtaani katika pilikapilika zangu za kawaida, njiani naona gazeti lenye kichwa cha habari Amina hatunaye tena. Nashangaa!. Namuita muuza gazeti na kununua gazeti kupata undani wa kilichoandikwa.Baada ya kusoma nathibitisha kuwa Amina Chifupa ameaga dunia. Hatunaye tena.

Kweli chema hakidumu!

Mithili ya Amina Chifupa ndani ya CCM sijamuona. Mfanao wa mpambanaji jasiri dhidi ya ufisadi miongoni mwa wa wabunge wa chama kinachotawala ukimuondoa Amina mwingine simjui.

Nikiwa nimepigwa butwaa, nachukua simu yangu ya mkononi, kufungua blogu ya ndugu Michuzi nakutana na habari inayoeleza kifo cha Amina Chifupa, ikieleza kuwa Amina amefariki usiku wa kuamkia jana saa tatu kasorobo katika hospitali ya jeshi Lugalo alikokuwa amelazwa.

Kweli duniani tu wapitaji. Mungu aipe nguvu familia ya hayati Amina Chifupa kustahimili katika kipindi hiki kigumu.

Ningeweza kuishia kutoa pole kwa familia,nikamaliza. Lakini kuna mengi ya kusema juu yake, kwa kuwa alikuwa akifanya kile ambacho watanzania tulipenda kumuona akiendelea kufanya. Kupambana na ufisadi unaotuzunguka. Tunakumbuka jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya madawa ya kulevya. Amina alithubutu kufanya yale ambayo wengi hawana ujasiri wa kuyafanya,kuiondoa hali ya hewa chafu inayotuzingira, alikataa kuiona harufu hiyo chafu kama hali ya kawaida.Alikemea, alihoji na alisimamama kwenye haki.Alikuwa mtetezi wa watu duni.Watu wa aina hii si wengi miongoni mwa viongozi wetu wa leo.Ni kweli kuwa ameacha pengo kubwa, ndani ya chama alichokuwapo, sijamuona wa kuliziba.

Binadamu tu wasafiri, maisha yetu duniani ni mafupi, na tuishi kwa kutende mema kwa jamii ituzungukayo, walio katika nafasi za uongozi na wawapende na kutenda haki kwa wale wanaowaongoza ili siku ya kuondoka itakapowadia matendo yetu mema yaendelee kuishi na jamii tuliyoiacha.

Wote tuseme mapambano yanaendelea.

Kwa heri mpendwa wetu

Sunday, June 24, 2007

Karibuni wote

Nawakaribisha katika blogu hii tuweze kendeleza harakati za kujikomboa dhidi ya maadui watuzungukao yaani ujinga, maradhi na umaskini pamoja na kila aina ya ufisadi unaoendelezwa na mafisadi ndani ya mfumo wa kifisadi.
Mapambano hayajaisha kwani ukoloni unaendelezwa kupitia mlango wa nyuma na unyonyaji bado ungalipo.Mtu duni anaendelea kuwa duni na mwenye nacho anaendelea kuwa nacho kwa kumnyonya mtu duni asiye na sauti.Bila usawa hakuna haki. Ni jukumu letu sote kuupigania usawa ndani ya jamii tuishiyo kwani binadamu wote ni sawa na wote tuna haki ya kuishi maisha bora.