Monday, June 29, 2009

BURIANI PROF HAROUB OTHMAN!

Kweli Duniani tunapita!

Taifa limepoteza msomi, mwanadiplomasia na mwanaharakati wa haki za binadamu ambaye siku zote aliwatetea wanyonge wa Taifa hili, Africa na Duniani kote.

Tutakukumbuka daima Prof Othman, nakuweka kundi moja na kina Prof Chachage kwa kuacha fikra zitakazoishi kwa muda mrefu ndani ya jamii yetu.

Kwaheri Prof Othman.

Saturday, April 4, 2009

SIJUI NIJARIBU UBUNGE?


Wapo wanaosema ndogo, wapo wanaosema zinatosha, wapo wanaosema ziko juu sana. Hata wao wenyewe wanatofautiana mfano ni 'ishu' hiyo hapo juu kama ilivyoelezwa na mbunge wa Karatu Dr. Slaa.
Mi nasema ni nyingi mno ukizingatia mishahara ya watu wetu bado iko chini sana, fikiria pale wahutimu wa vyuo vikuu wanaolipwa mshahara wa laki tatu na nusu. Kwa mbunge anayepata 6,900,000/= kwa mwezi kipato chake ni sawa karibu mara ishirini ya kipato anachopata mhitimu wa chuo kikuu.
Kwa maelezo yoyote yale,hii si sawa!

Thursday, March 26, 2009

TUTAANZAJE UPYA BILA FIKRA MPYA?

Mijadala ni mwanzo wa kuibuka kwa fikra mpya na changamoto kuelekea maendeleo ya kijamii. Pasipo mijadala mawazo yamefungwa, yanabaki vichwani tu. Mijadala isiyokamilishwa na matendo ya kuyatekeleza ni mijadala iliyokufa.Haitufai.

Ni dhahiri yako mengi yasiyo sawa, ndani ya jamii na yanayotuzunguka, ndani ya daladala, radioni kunasikika hotel ya Paradise imeungua, iko Bagamoyo.Bagamoyo gari ya zimamoto hakuna, jamaa anaongea kwa sauti kuuuubwa, anauliza “gari moja ya zima moto shilingi ngapi hata kuishinda wilaya kama Bagamoyo kulimiliki”? Hotel imeungua. Imeteketea. Hatuoni. Hatusikii. Hatubadiliki.

Hapa ndipo watu wanajiuliza,” ni nani aliyeturoga?”, tuangalie kwa uchache baadhi ya mambo.

Elimu yetu, ni kwa vipi inatusaidia kutatua matatizo yetu?, ni kwa vipi inaikabili hali ya umaskini inayotuzunguka?, ni kwa vipi imejipanga kukabilianana mahitaji halisi ya jamii yetu?, ni kwa vipi inapunguza pengo la kiteknolojia lililopo kati yetu na mataifa yaliyoendelea litufanyalo tuendelee kuwaabudu ‘wazungu’ kuwa wenye akili sana kana kwamba waafrika tumezaliwa tukiwa ni “vilaza”?, Inawaandaaje watu wetu kuwa wavumbuzi siku zijazo?, Inawaandaaje watu wetu kulima kilimo cha kisasa?, Inawaandaje watu wetu kujikinga na maradhi kama malaria na kipindupindu?,
Ni kwa vipi imejipanga kukabiliana na mahitaji halisi ya jamii yetu?, tunaambiwa waalimu tulionao ni wachache, nini kinafanyika kuondoa tatizo hili?, na kama kuna linalofanyika ni kwa ubora gani?. Kuna wakati ilikuwa fahari kusoma shule za Serikali kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.Hali si hivyo sasa. Aanyebisha na ajitokeze!. Watu wenye uwezo wa kifedha hawapeleki wana wao kwenye shule hizo.Viongozi wetu hawapeleki wana wao shule hizo. Zimekuwa shule za kina Kayumba!, Wenye uwezo wanasomesha wana wao shule za seminary, shule za mtakatifu fulani na fulani, wakilamaliza wanawapeleka vyuo vya nje.Wanatudanganya kwa kuonyesha uzalendo wao kwenye kuchangia mabati ya shule na madawati. Mbona watoto wao hawasomi huko?, Kwa nini tusiwaambie wabunge na madiwani wetu kuwa kama watoto wenu hawasomi shule zetu na nyinyi si wenzetu?, kama watoto wao wangesoma shule zetu, zingekosa walimu?, zingekosa madawati?, wasingezijali?
Turudi kwa walimu, nani asiyejua kuwa huu ni uchaguzi wa mwisho wa wanafunzi wetu wanapokosa vyuo vingine vyooote!, hii imepelekea wanafunzi wanaopata daraja la nne ndio hufikiria kuomba kudahiriwa kwenye vyuo vya ualimu.Bado tunadhani tuna elimu bora?
Mbali na hapo waalimu hao wachache na baadhi wenye ubora mdogo wanahama taaluma yao muda mfupi baada ya kukabiliana na ugumu wa mazingira ya kazi wakiwa ndani ya ajira zao

Uchumi wetu, madini tuliyonayo kwa uchache tukitaja dhahabu, almasi na tanzanite bado hayajatuletea tija ya kutosha. Mwalimu Nyerere aliwahi kutuasa kuwa tuyaache madini yetu hadi pale tutakapoweza kuyachimba wenyewe kwa kutumia wataalamu wetu. Wajanja wakaja na pipi wakatuzidi akili tukawaachia, eti wawekezaji.Wizi mtupu!.Tunaambiwa wanatuachia 3% tu ya mapato, na sisi ndio wenye mali. Si wizi huo?. Geita,Tulawaka, Bulyankulu, Buzwagi, Kahama, North Mara iko siku tutashuhudia mashimo mareeeeeeeefu, sijui tutawajibu nini wana wa wanetu pale watakapotuuliza kilichotoka kwenye mashimo hayo tulikiuza wapi, shilingi ngapi na tulitumiaje kilichopatikana?. Bila shaka uwekezaji ( niuite wizi) huu uliofanyika katika madini yetu mithili ya huo duniani haupo!.Tunaambiwa mmmoja wa mikataba hiyo ulisainiwa Uingereza na waziri husika.Inasemekana shughuli hiyo ilifanyika hotelini. Nani aliyeturoga watized sie?

Samaki, ndio tumeibiwa mpaka basi. Majuzi kuna meli imekamatwa na tani 200 za samaki, kilo moja ni dola 20, tani 200 ni kilo 200,000, hivyo gharama ya wizi ule uliozuiwa ni 4000,000$, kwa kiwango cha kubadilisha dola cha sasa 1300/=, tungepoteza billioni 5.2 fedha za kitanzania. Wajinga ndo waliwao, duh!, wale wachina, wavietinam,ufilipini, indonesia na wakenya watatu, arobaini yao ilikuwa imefika, kesi iko mahakamani sasa. Kazi kwao.Kabla ya hizo arobaini zao, anzia moja, mbili, tatu,……… hadi arobaini, ni shilingi ngapi zilizoibiwa?, kama ndio ilikuwa kamchezo kao jamaa, tuwapigie hesabu 40-1=39; 39 zidisha kwa bilioni 5.2 ni sawa na bilioni 202.8/=.Wizi mtupu!. Tones na tones za samaki wetu wa baharini na maziwani zinaenda Ulaya.Uwiano wa mapato na kinachochukuliwa ( kinachoibwa) ni mdogo saana!. Maziwa na bahari zetu nazo ni shamba la bibi?, kila mtu anavuna na kula!, bibi hana noma!,eti wacha wajukuu wale!, tuseme nini basi kama si kulogwa ni nini?. Nani wa kutukomboa na giza hili?.Hakika bado tungali gizani hata katika mwanga huu!
Wako wapi wenye taaluma ya viumbe hawa wa majini?, Je tuna mabaharia wa kutosha katika shughuli hizi za majini?, Ulinzi wa majini uko bora kwa kiwango kinachostahili?, walikovua samaki wetu hao wezi, je sisi tuna meli gani tunazozitumia kuvua huko?,Au kuvua hatuvui samaki wetu lakini kuibiwa hatutaki?

Maadili yetu, hapa napo panazingua!. Sielewi ni nani mlinzi wa maadili yetu kama si sisi wanajamii wenyewe?, nani anayekemea mmong’onyoko wa maadili unakwenda kwa spidi ya swala katika jamii yetu?, Waangalie dada zetu, ni uchizi kama si uwendawazimu, hakuna nguo za siri tena kwani leo hii ni kawaida kuwaona mabinti wamevaa chupi zikiwa juu ya suruali zao za kubana, wanazionyesha za nini?, wanamuonyesha nani?,ili iweje?. Nguo fupi na viblauzi vya kuishia juu ya kitovu, eti fashion.Sijui. Ila nionavyo tuendako hakuna maelezo ya kutosha kuelezea yatakayojiri kwa wana na wana wa wana wa taifa hili! Mashuleni na vyuoni ndipo yalipotamalaki mambo hayo wanayoita ‘kwenda na wakati’!

Naungana na wanaosema tunahitaji mijadala ya kitaifa katika kutatua matatizo yanayotuzunguka.

Tufanye hivyo!.

Tuanze sasa!

Mijadala hujenga fikra!

Mungu ibariki Tanzania!

Wednesday, March 25, 2009

BILLY GRAHAM AND US PRESIDENTS!

David Frost ndiye muandishi, ni habari inayoeleza nyuma miaka 30 Mazungumzo yao na Billy Graham katika kitabu kiitwacho “Personal thoughts of a public man”

Billy Graham ni mhubiri wa kimataifa, anafahamu siasa za Marekani na amekuwa rafiki wa karibu wa karibu kila raisi wa taifa hilo kubwa kama vile,Harry Truman, Eisenhower, Lyndon Johnson ,John Kennedy, Richard Nixon na Bill Clinton.

Ukurasa wa 95
President Bill Clinton, May 6, 1996 alinukuliwa akisema:

‘I hardly ever go to a place, as Presiident, that Billy Graham has not been there before me preaching. And I feel like a poor substitute, because a lot of the time what I’m trying to do is to get people to lay down the hatred of the heart and reach down into their spirit and treat people who are different from themselves with the same respect that all God’s children are entitled to…………………..
I thank Billy and Ruth Graham for the ministry of their lives’

Ukurasa wa 97;

David Frost, mwandishi wa kitabu hichio: anasema ‘No preacher in the history of this country has had so much access to many presidents as Billy Graham’.



Hapana shaka kuwa alikuwa mshauri wa kisiasa wa wakuu hawa wa Marekani, ushauri uliobeba ukweli na sera zenye kubeba haki na demokrasia.

Marekani ya leo inayoongozwa na Rais Obama, mweusi, ni dhahiri kuwa ni mwendelezo wa harakati fulani za hadharani kama za kina Martin Luther na kina Billy Graham.`

Hapa tunajifunza kuwa viongozi waongozao roho zetu wana nafasi kubwa ku ‘influence’ siasa zetu, hapa Afrika na hasa Tanzania katika kujenga jamii bora zaidi,yenye hofu ya Mungu na kusimamia haki. Na si kuendekeza ufisadi unaolimaliza bara la Afrika. Mfano mzuri wa mapambano haya na harakati za kuipigania haki ni Askofu Desmon Tutu wa Afrika ya kusini. Ambaye wakati Mandela akiwa gerezania alionekana hadharani akiongoza maandamano ya kuidai haki ya usawa ndani ya nchi yao na kuna wakati aliwakemea watawala wa Afrika a kusini, wabaguzi,, kwa sauti kuuuubwa “ Release our leaders”, “Release our leaders”, “Release our leaders”. Bado watanzania tumo katika kifungo cha umasikini, maradhi, ujinga, ufisadi. Nani wapigao kelele mithili ya Desmond Tutu akiwataka watawala wetu na wakoloni wetu wa kale kutuacha huru.


Wako wapi kina Billy Graham wetu Tanzania!

Friday, January 23, 2009

RWANDA ARRESTS REBEL LEADER




Gen Nkunda has said he protects Congo's Tutsis from Rwandan Hutus
Gen Laurent Nkunda, leader of the strongest rebel group in eastern Democratic Republic of Congo, has been arrested in Rwanda.
He crossed the border after resisting a joint Rwandan-Congolese operation to arrest him, both countries say.
Correspondents say it is a startling about-turn by Rwanda, which had been accused of backing Gen Nkunda.
The BBC's Thomas Fessy says there is a sense of relief among residents in Goma who feel the war is nearing an end.
Some 250,000 people fled their homes in the region when Gen Nkunda led an offensive on the city towards the end of last year.
Some 4,000 Rwandan troops entered DR Congo this week to help fight rebel forces in the area.

See detailed map of the area Correspondents say Gen Nkunda's arrest removes one obstacle to peace but other rebel groups remain active.
The UN refugee agency warns that further military action against other rebel groups in the area could lead to a humanitarian disaster.
BBC Africa analyst Martin Plaut says Gen Nkunda has been caught in the rapidly changing diplomatic situation in Central Africa.
LAURENT NKUNDA
Age: 40
Congolese Tutsi
Fought for Tutsi rebels in Rwanda and DR Congo
Accused of war crimes in DR Congo
Studied psychology
Owns a cheese farm
Gen Nkunda had been Rwanda's ally in eastern DR Congo - a Tutsi, like Rwanda's leaders, he guarded their western flank against attacks from the Hutu forces who fled there after the Rwandan genocide of 1994.
But in mid-November Rwanda shifted its position, announcing it would work with the Congolese to destroy the Hutu rebels.
Gen Nkunda did not back the new alliance and so became an impediment to Rwandan plans in the region, causing Rwanda to turn on him, our correspondent says.
The decision earlier this month by a group of Gen Nkunda's top commanders to break away and join forces with government troops gave them their opportunity, he adds.
Henry Boshoff, an analyst from South Africa's Institute for Security Studies, told the BBC that following intense diplomatic pressure in recent months, Rwanda was obliged to arrest Gen Nkunda.
The next step is for the joint Congolese-Rwandan force to tackle the FDLR Hutu rebels, some of whose leaders are accused of involvement in the 1994 slaughter in Rwanda of some 800,000 Tutsis and moderate Hutus.
But Mr Boshoff says this may not be easy, as they have resisted previous attempts to disarm them.
Arrest warrant
The rebel leader was detained in Rwanda after troops converged on his stronghold in the Congolese town of Bunagana.
"The ex-general Laurent Nkunda was arrested on Thursday 22 January at 2230 hours while he was fleeing on Rwandan territory after he had resisted our troops at Bunagana with three battalions," a Congolese-Rwandan official statement said.

Gen Nkunda has lost the support of some of his troops in recent weeks
Rebels with him were being urged to disarm, reports said.
Congolese Information Minister Lambert Mende Omalanga, told the BBC he welcomed the arrest.
"I think it is a good achievement for peace and security in this area and this region of Great Lakes," he said.
Mr Omalanga said he wanted Rwanda to extradite him to face justice in DR Congo.
DR Congo has issued an international warrant for Gen Nkunda's arrest following past accusations that his forces had committed atrocities.
Rwandan army spokesperson Major Jules Rutaremara told the BBC that General Nkunda was being held by the Rwandan forces in Rubavu district in western Rwanda, close to the border with the DR Congo.
But the Rwandan authorities have not yet issued any formal statement concerning his arrest.
Some of Gen Nkunda's forces - perhaps as many as 2,000 - are still said to be loyal to him.
The question now is whether they will fight, or whether they will join the new consensus and become integrated into the Congolese army, correspondents say.
The CNDP launched a major offensive in August 2008, which displaced more than a quarter of a million people in North Kivu and raised fears of both a humanitarian crisis and a wider regional war.
Correspondents say this may have been Gen Nkunda's undoing, by bringing huge international pressure on all sides to end the conflict in DR Congo.
Human rights group have accused CNDP forces, along with those of the government, of numerous killings, rapes and torture.
All sides in the Congolese conflict have also been accused of using the fighting as a pretext to loot eastern DR Congo's rich resources of minerals such as gold, tin and coltan, used in mobile phones.
Some five million people are estimated to have died as a result of almost 15 years of conflict in DR Congo, following the Rwandan genocide.
Source:BBC News

Tuesday, January 20, 2009

US PRESIDENT BARACK OBAMA!

Obama will soon be declared as a 44 US president, the history will write his name in the mind of young men and women of this day, old men and women of this day and school children of this day!

The dream of Martin Luther King is coming true this day!
To some of us inauguration of 44 US president, a black man,Obama, is speaking aloud one thing, that is "It doesn't matter you are born white or black, we all have equal rights to all opportunities around us"

Wishing him all the best!



Tuesday, December 2, 2008

TUWAKATAE VIONGOZI WACHAFU,WALAFI NA MAFISADI!!

Hakuna lisilowezekana katika sayari hii izungukayo!Kila jambo lina wakati wake, wakati hubadilika, binadamu hana budi kwenda na mabadiliko hayo vinginevyo atabaki nyuma na kuachwa na wakati.Kwa muda mrefu Afrika imefanywa kuwa nyuma kutokana na uongozi mbaya wa viongozi walafi wapenda madaraka, wenye utajiri wasioweza kuutolea maelezo, walioupata kutoka kwa kidogo kilichopaswa kuwafikia wananchi wao.

Kile kidogo ambacho kingeweza kuinua maisha ya wananchi wao wamekibinafsisha, ni mithili mfugaji mwenye kutamani kupata ongezeko la maziwa kwa ng'ombe wake bila ya kumuongezea lishe,kumtafutia majani mabichi, wametamani kukamua ng'ombe maziwa yote hata waone matone ya damu, na wametamani maziwa hata kwa ng'ombe dume!!!!

Afrika ambayo imepigania uhuru wake kuanzia miaka ya hamsini bado haijawa huru kiuchumi hata kifikra!!, wako wapi mashujaa wetu wa leo?

Wako wapi kina Julius Nyrere, Kwame Nkrumah, Samora Machel, Nelson Mandela wa leo?, ni lini walikoma kuzaliwa ndani ya Afrika viongozi mithili ya hao?, Bado tunashuhudia Afrika ikiliwa kwa nje na nchi tajiri na kwa ndani na viongozi walafi, hali ikiwepo kasi ndogo na sheria iliyolegezwa na nguvu ya pesa kuwazuia wailao kwa ndani pamoja na kukosa ujasiri wa kupambana na wale wailao kwa nje.

Mwalimu Nyerere wakati akizitetea nchi za dunia ya tatu, alipata kuwakemea mabepari, nchi tajiri,walipokuwa wakishinikiza tuwalipe madeni yao, hela waliiyotunyonya na kutukopesha, akawaambia ni sawa na kumtoa damu mgonjwa mahututi,Afrika iko mahututi kichumi bado!!, wazungu wale walimuelewa Mwalimu!!, Ni nani anayeendeleza mapambano hayo kwa kasi ile ile leo?

Leo tunaona jinsi siasa inavyokimbiliwa hata na wanataaluma, wanajua ni rahisi kuneemeka ukiwa huko,hasa kwa walio na dhamiri zilizokufa,wanaothubutu hata kuchota mapesa ya kununua madawa na kununua magari ya kifahari!!, wanasayansi wamekimbilia siasa, kwa staili hii maendeleo yakujaje?

Kuna ujasiri mwingi na thubutu kubwa ambayo viongozi wetu walio safi wanapaswa kutuonyesha, na wasipofanya hivyo, basi umma utawalazimisha kwani wakati wa mabadiliko ukifika hakuna awezaye kuuzuia, na atakayejaribu kufanya hivyo atakuwa anapambana na nguvu kubwa asiyoiweza!!

Hapa Tanzania tumeshuhudia mawaziri wawili Basil Mramba na Daniel Yona wakipandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya jinsi walivyotuibia, tunahitaji mwendelezo wa mapambano haya dhidi ya wale wailao nchi nyetu kwa ndani kwani ni wengi na wasiopaswa kuongoza kwa wakati wa sasa!!

Tuwakatae kama Mwalimu alivyotuasa!!!

Tuko kwenye zama nyingine kabisa,, hakuna lisilowezeakana!!!!!

Wednesday, November 5, 2008

CONGRATS OBAMA!

OBAMA, the first black US President, Conratulations to Americans to go beyond racism.

Sunday, October 26, 2008

MOGAE OYEEEEEEEEEEEEEE!

Heko Mogae, Rais mstaafu wa Botswana kwa tuzo ya Mo Ibrahim.Mogae ndiye mshindi wa mwaka 2007 na amejinyakulia kitita cha dola milioni 5 ikiwa ni pamoja na dola laki 2 kila mwaka hadi atakapoondoka duniani.

Ndio, malipo ni hapahapa duniani, alitenda mema kwa watu wake na amelipwa mema kwa aliyotenda!

Laana nayo ni hapahapa duniani, tazama jinsi viongozi wetu matapeli, walafi, walevi wa madaraka, mafisadi na kila aina ya uchafu waondokapo madarakani, ni aibu tu inayobakia kwao kiasi cha kukosa ujasiri tena wa kuishauri jamii waliyokuwa wakiiongoza!

Mogae alipambana na rushwa akapata mafanikio, alipambana na ukimwi akapata mafanikio.Huyu ni Festus Mogae wa Botswana aliyewabwaga wenzake kina Benjamin Mkapa wa Tanzania,Olusagan Obasanjo wa Nigeria na Ahmad Tejan Kabbah wa Siera Leone.

Mwaka 2007 mshindi alikuwa ni Joachim Chisano wa Msumbiji, mwaka 2008 amekuwa ni Festus Mogae. Je miaka michache ijayo baada ya raisi wetu kuachia kiti kuna matumaini yoyote ya kuibuka kidedea?
Kama Mogae na Chisano wameweza kupambana na matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kupata mafanikio, Kikwete anashindwa nini?

Ingawa yawezekana ikawa muhimu si zile fedha wanazopata bali kutambulika kwa yale mema waliyoyafanya na kubakia kuwa viongozi wa kuigwa!

Yapo matatizo mengi yatuzungukayo!, rushwa,mikataba ya kifisadi,wizi wa EPA, ukimwi, ujinga, umaskini, gharama kubwa za uchangiaji elimu ya juu na mengine kibao!

Kadri miaka ya utawala wa awamu ya nne inavyoondoka tunataka kuona mabo hayo yakipungua kabisa kama si kwisha.Kinachotakiwa ni kuthubutu na kudhamiria kwa ujasiri mkubwa.

Inawezekana!

Huu ni ujumbe wangu kwako Mr President!

Sunday, March 23, 2008

HERI YA PASAKA!

Leo tunaazimisha kufufuka kwa Bwana Yesu miaka 2000 iliyopita,jambo la kujiuliza ni kwamba, kufa na kufufuka kwake Bwana Yesu kumeleta nini katika maisha yetu?, kumeyabadilisha vipi maisha yetu?
Tutafakari.
Baada ya kutafakari na kujibu maswali hayo tusherekee kwa matokeo ya siku hii ya kusherekea kufufuka kwa Bwana Yesu.
Kufufuka kwake kulileta ukombozi wa miili na roho zetu!
Ni siku ya kumshukuru Mungu kwa hilo na kuyapa kisogo mambo yaliyo maovu!
HERI YA PASAKA!!!

Sunday, February 10, 2008

TANZAINIA BILA UFISADI INAWEZEKANA!

Nimeisikiliza ripoti ya kamati teule ya bunge iliyochunguza kampuni iliyopewa zabuni ya kuzalisha umeme, Richmond. Mwenyekiti Mwakyembe katuambia haikuwa na uwezo hata wa kuchomeaka taa kwenye kishikio (bulb holder) chake. Huu ni mzaha mkubwa kwa watanzania, wakuu wale waliopitisha kwa kulazimisha mkataba ule, ripoti ilielezea kama ni watu wenye ujasiri wa kifisadi.Hakika ndivyo walivyo.
Ni kashfa kubwa ambayo Lowasa kwa nguvu ya madaraka yake alishindwa kuizima, kwani kamati iliyoshughulikia swala hilo ilikuwa makini kweli kweli.
Kama ambavyo bunge limeomba mikataba yote sasa iende bungeni ijadiliwe, wahusika si tu, wawajibishwe bali wafilisiwe na washitakiwe!
Ikiwa jamii huapata hasira kwa wezi na vibaka waibao kuku mitaani au kuchoa simu mifukoni kiasisi hata cha kuwachoma moto iweje hasira hiyo ishindwe kuwawakia mafisadi hawa wanaoiba mabilioni yetu?, Moto unaowastahili hawa si wa kiberiti ni maisha ya jela kwani waikosea jamii na wamezidi kuifukarisha jamii yetu na kurudisha nyuma mapambano dhidi ya umasikini!
Tunahitaji kina Mwakyembe kumu tu kuibadili nchi hii ambayo tayari ilishaanza kuoza na kunuka kwa ufisadi.
ALUTA KONTINUA!

Friday, January 4, 2008

IS IT DEMO-CRACY OR DEMO-CRAZY?



Another shame in Africa!!!
As an East African, i am deeply sympathetic of what is going on in Kenya!!, aah!,what is wrong with Africa?. Every one could see that something was wrong in the whole process of counting the votes!,only re election will clear the doubt,in this Kibaki has no choice, re counting may not give something different, anyway let the Kenyans decide!, we don't want to see more blood of our fellow Africans.
We want peace in Kenya.
We want peace in East Africa.
We want peace in Africa!

Tuesday, December 25, 2007

Wednesday, October 24, 2007

GAZETI JIPYA RAIA MWEMA!

Moja ya magazeti ambayo nilitokea kuyapenda kwa muda mrefu sana ni gazeti la Rai.Hii ilitokana na umakini na ujasiri wa waandishi wa gazeti hili.Ninaamini kabisa kuwa magazeti yana sehemu kubwa katika kujenga fikra zetu, kutufundisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutuonyesha uozo, au tuuite ufisadi, ndani ya jamii yetu na hata namna ya kupambana na uozo huo. Magazeti yakiandika habari za kweli na kwa uwazi yataweza kuisaidia jamii yetu kusonga mbele kifikra na kimaendeleo.

Nakiri kwa kusema kuwa hamu ya kulisoma gazeti la Rai imenitoka,siku hizi nalinunua kwa mazoea tu, umakini na uandishi wa gazeti hili sio ule wa walipokuwa wakiandika akina Jenerali Ulimwengu na Maggid Mjengwa.Nadhani sasa gazeti hili jipya la “Raia Mwema” litaziba pengo lililoanza kujitokez andani ya Rai, sijui gazeti la Rai limekumbwa na nini.Sielewi!

Muda mfupi nimeisoma habari ya kuanzishwa kwa gazeti hili, na wiki ijayo inatoa toleo la kwanza, miongoni mwa waandishi ni Jenarali Ulimwengu, Prof Issa Shivji,Maggid Mjengwa, Mihangwa na Padri Pivatus Karugendo.Kama unawafahamu waandishi hawa basi usikose kusoma makala zao!.Utaniambia mwenyewe!

Sina shaka na hawa waandishi kuwa kuwa wamekubuhu katika taaluma ya uandishi wa habari, watakuwa na ujasiri wa uandika yale ambayo wengine wameogopa, watashiriki katika mchakato wa kuisafisha jamii yetu inayoendelea kuchafuliwa na ufisadi, utandawizi na mmong’onyoko wa maadili.

Kila la kheri gazeti la “RAIA MWEMA” ninaahidi kukunua kila utokapo!

Sunday, October 21, 2007

WATU WAOVU WAMEMUUA LUCKY DUBE!

Ni mchana wa ijumaa niko sehemu napata msosi wa mchana, pembeni jamaa anaongea na mwenzake, Lucky Dube amefariki, nayasikia maongezi yale, kwa kuwa sikuwa mbali na meza yao.Nashangaa!.Namuuliza mmoja wao , ananiambia ni kweli jamaa wamemuua Lucky Dube.Jioni siku hiyo hiyo ya ijumaa nasikiliza Voice of America, nasikia wanatangaza kuwa Lucky Dube ameuwawa.

Nikiwa njiani nakutana na ajali daladala,DCM, imeuvaa mti, mtu mmoja amefariki, mwili wake ukiwa bado umelala barabarani!
Maisha ni safari yenye mwisho,hakuna ajuaye mwisho huu unafika lini!,Lucky Dube hakujua kama siku ile angeaga dunia,watu wasio na utu wamemuua, ni watu wenye dhamiri zilizokufa tu, ndio wawezao kufanya kitendo cha kinyama kiasi hicho!

Kijana yule angejua kuwa gari lile lingepata ajali asingalipanda daladala lile!,kifo ni kitu ambacho tumefichwa tusijue kinakuja lini na kwa staili gani!
Anyaway, maisha hayana budi kuendelea!

Ni aina ya uaimbaji wake na ujumbe ndani nyibo zake ndizo zinisukumazo kuandika juu yake.South Afrika na Afrika kwa ujumla imempoteza
mpambanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi,mwanamapinduzi na mpigania haki za watu wanyonge Lucky Dube!

He has gone but the messages in his songs will continue to live!

Sunday, October 14, 2007

NYERERE DAY

Ninaikumbuka siku hii ya leo, miaka 8 iliyopita, tarehe 14 october 1999,nikiwa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha Dar es salaam, kitivo cha uhandisi, nakumbuka tulikwa kwenye kipindi katika karakana ya umeme. Mara tukasikia wimbo wa taifa unapigwa,kila mmoja anaikimbilia radio kisha tunamsikia raisi wa awamu ya tatu,Mkapa anatangaza Mwalimu Nyerere amefariki dunia! Baada ya muda uongozi wa chuo unatoa tangazo la kusimamisha ratiba zote za vipindi.Ilikuwa mshtuko mkubwa.Baada ya siku kadhaa mwili unawasili Tanzania chuo kikapanga utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanachuo kwenda kuuaga mwili wa hayati Mwalimu Nyerere,nilikuwa mmoja wa waliofika uwanja wa taifa kuuaga mwili wa Mwalimu, usiku wa manane lakini ilikuwa kama mchana jinsi watu walivyojaa.Umati ule unanifundisha jambo moja 'kuongoza ni kujitoa kwa ajili ya unaowaongoza', Mwalimu aliyatoa maisha yake kwa ajili ya taifa lake, aliishi alichokisema na alisema alichokiishi tofauti na viongozi wetu wa leo!

Tunapoikumbuka siku ya kufariki kwa Mwalimu Nyerere hii leo tujiulize maswali yafuatayo:-

Hivi mwalimu angalikuwepo soo kama la Richmond Development Cooperation lingepita kimizengwe vile na mambo yakaisha kiaina kama yalivyoisha?
Sasa tunaambiwa kuwa mkataba ule ulisainiwa usiku na Tanesco hawajui ni nani aliyeusaini. Inashangaza!

Hivi ule mkataba tata wa madini wa Buzwagi ungepita hivihivi bila kuundiwa tume huru aliyoiomba Mbunge Zitto?
Bila shaka Mwalimu angemwagia sifa Zitto Kabwe hadharani na kuwasuta wabunge wa CCM waliomfukuza bungeni.Bila shaka angesema kuna haja ya waziri Karamagi ajiuzulu!

Hivi ile kashfa ya ufisadi aliyoiibua Dk Slaa, wale waliotajwa angelipuuziwa kama ambavyo wanafunzi wake wamepuuzia? Bila shaka angaliwaita wote Butiama na kuwahoji maswali magumu, na labda angalishauri baadhi yao wajiuzulu!

Hivi Mwalimu angalikuwepo wanafunzi Mlimani wangelipishwa 40% ya ada? Bila shaka angalikemea kwa nguvu zote!

Huyu ndiye Mwalimi ambaye miaka nane sasa bila yeye viongozi wetu wameshindwa kuweka dhamira yao kwa dhati na kwa vitendo kupambana na ufisadi, kwani hata ndani ya chanma alichokiasisi yeye Mwalimu nguvu ya pesa inatumika kupata uongozi!

Miaka minane bila Mwalimu Nyerere ujumbe kwa viongozi wetu ni kuwa, wamuenzi Mwalimu kwa vitendo na si kwa maneno kama wafanyavyo sasa,tumechoshwa na porojo, tumeschoshwa na maneno tunataka vitendo.

Friday, September 28, 2007

HOJA YA KUANZISHWA BLOGU YA WABUNGE NA WANANCHI!

Mara nyingi katika mijadala isiyo rasmi ninayoifanya na watu mbalimbali tunapojadili mambo ya siasa tunakubaliana kuwa tatizo kubwa la siasa ya nchini kwetu ni mfumo mzima unaoendesha siasa.Ni kama vile wananchi hatuna sauti na nguvu ya kuwaaambia wawakilishi wetu bungeni kuwa ni nini tunataka, na wao wakakisimamia kuhakikisha kinafanyika, kwa hali ilivyo sasa ni kama vile wabunge hatujawatuma wametumwa na chama hasa wale wa CCM.Wanasikiliza zaidi chama kuliko wananchi wanaowawakilisha.Mfumo huu haufai na tunaweza kuurekebisha.

Hivi kwa nini kusiwe na blogu, mfano www.wasiliananawabunge.blogspot.com, ambayo itawakutanisha wananchi na wabunge,kabla ya wabunge kwenda Dodoma na wakati wakiwa Dodoma tuwaeleze nini waihoji serikali kwa niaba yetu, na tusiporidhika wakiwa huko huko Dodoma tuwaeleze hatujaridhika na majibu ya Serikali ili wahoji, wahoji na wahoji hadi majibu yapatikane.Vinginevyo tutaendelea kusikia majibu ya porojo ya kila siku wanayojibu mawaziri wetu ,yasiyo na nguvu ya uwajibikaji, majibu kama, serikali iko mbioni kushughulikia swala x,serikali inafuatilia kwa karibu suala y,serikali ina mkakati wa kufanya swala z,serikali imejizatiti kuondoa uasikini ifikapo mwaka f,serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kero h inakwisha, majibu haya hayatoshi na yanahitaji maswali mengine zaidi lakini wabunge wetu huridhika nayo.

Wakati umefika sasa wa kuwa na jukwaa la kuwaambia wabunge wetu pale tunapotaka waihoji serikali na tusiporidhishwa na majibu ya serikali.

Blogu hii pia iwe na e mail address na namba za simu za wabunge wote.

Tutaendelea kuyanyoosha yaliyopinda, hadi pale yatakaponyooka.

Hoja hii ninaikabidhi jumuiya ya wanablogu Tanzania, JUMUWATA, ikifaa ifanyiwe kazi na isipofaa itupiliwe mbali.

Naomba kuwasilisha!

Thursday, September 27, 2007

WABADILIKE WATUTUMIKIE AU WAJIUZULU WAKALIME

Wakati tuliousubiri haukuwa mbali sana kama nilivyofikiri, wakati huo si tu kuwa umekaribia bali umefika.

Kila kilichofichwa kichakani kitawekwa juu milimani na kila kilichofichwa gizani kitawekwa kweupe nuruni, ili kila mwenye macho aone.Bonyeza hapa uone yale yaliyofichwa ambayo Dk Slaa ameyafichua, tunamshukuru Mwanakijiji kwa kutuwekea ripoti hii ya Dk Slaa.

Hatuwezi kuufumbia macho ubadhirifu unaotendwa na viongozi wetu,hawa mafisadi wanaoutenda na wajue sasa kwamba siku zao zinahesabika, kwa kuwa viongozi wao waliowateuwa wanawahifadhi na kuwaonea aibu kuwawajibisha sasa wananchi wanawaanika kweupe, wachague sasa kujiuzulu na kwenda kulima au kubadilika na kuwatumikia wanachi kwa uaminifu.

Wasidhani tumelala tunawaangalia kwa macho mawili.

KISWAHILI NA KIINGEREZA KIPI ZAIDI?

Bila shaka usomapo unajibu la swali hapo juu?, najiuliza tu.Waafrika tuna kaugonjwa fulani kakudharau cha kwetu. Ndio.Yawezekana ni athari za ukoloni, waliviita vya kwetu vya kishenzi nasi tukaviona hivyo na kuvitukuza vya kwao na hii iko hadi leo.
Hii imepelekea kuiga kila cha mzungu, angalia leo utamaduni wetu ulivyopindapinda, haueleweki,sijui ni nini utambulisho wa mtanzania wa leo.Mimi nadhani ni Kiswahili chake tu!

Angalia dada zetu vivazi vyao, kuna wakati kulikuwa na uvumi kuwa presidenti wetu kapiga marufuku aina fulani ya vivazi vya dada zetu,wao wanaita vya kizungu,wengine waita vya kihuni!, jamaa wakazua kuwa mgambo watatanda na bakora halafu aonekane binti na kivazi cha kutatiza,analamba viboko kadhaa kama adhabu na onyo.Siku moja waandishi wa habari wakapata upenyo wakamuuliza mkuu, akajibu hana mpango wa kuchukua hatua hiyo, hayo ni mambo ya fashion tu, yatapita kama zilivyopita suruali za chini nimwagie miaka ileeeeeeeee. Vijana wa kiume wa kileo nao wamekuwa wazungu, wanasuka nywele, suruali zinavaliwa chini ya matako, ati mambo ya kizungu!.Mambo ya kuiga hayo!
Ni kwa vipi tutaweza kuulinda utamaduni wetu ulioingiliwa na utandawazi?

Leo hii tunaona kiingereza ni bora kuliko Kiswahili, tunaona hakifai kutumika kama lugha ya kufundishia, kama lugha inayofaa kutumika maofisini.Je tatizo hili ni la lugha au wenye lugha?.Si kuwa lugha ya kiswahili haiwezi kubeba kazi hizi, wenye lugha wameidharau lugha yao wamekitukuza kiingereza zaidi.Yawezekana kuwa lugha hii ina mapungufu lakini upungufu huu hauhalalishi kutokufaa kwa lugha hii, upungufu huu ni changamoto kwa wataalamu wetu wa kiswahili waweze kukiwezesha kiswahili kujitosheleza kutumika, mitaani kuwasiliana, mashuleni kufundishia, maofisini kwa mawasiliano ya kikazi.Wataalamu wetu watafsiri kwa kiswahili fasaha kila kilicho kwa kiingereza kiandikwe kwa kiswahili, kila kitu, vitabu vya mashuleni,maofisini,sheria zitumikazo mahakamani, vitabu vya maelekezo kwa wakulima juu ya matumizi ya mbolea na umwagiliaji,mikataba yote nchi hii inayoingia itafsiriwe pia ili wale wasio ijua lugha ya kiingereza waelewe yaliyoandikwa.

Kuna mwalimu wangu mmoja alinifundisha hesabu, tuition, enzi hizoooooooooooo, alijulikana kwa jina la ‘Mr So Much’, anasagia kwelikweli kiswahili anasema hakifai, anatupa mfano, anasema, kama kiswahili kingetumika kufundishia ingekuwa taaaabu kwelikweli, anatoa mfano, hapo anafundisha topic ya calculus, differentiation, sentensi kama ‘we differentiate y with respect to x’,dy/dx, tungesema ‘tunanyambulisha x kwa heshima ya y’, hapo hoja yake inakuwa kiswahili hakitoshi kufundishia na anatushawishi.Kwa wakati ule alitushawishi wengi tukakubali kuwa kiswahili hakifai kufundishia.Nadhani kina mapungufu yanayohitaji kurekebishwa na kuboreshwa.

Ukweli ulio wazi ni kwamba kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kuelewa masomo yao darasani na kufaulu usahili wanapoomba ajira.Endapo Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia kitamuwezesha mwanafunzi kuyapokea maarifa anayopewa na mwalimu wake kwa urahisi zaidi, ilivyo sasa mwanafunzi inabidi amsikilize mwalimu, atafsiri kinachofundishwa kutoka kiingereza kwenda kiswahili,akifanyie kazi akilini na kukihifadhi kwenye ubongo.Akishindwa kutafsiri alichosikia atashindwa kuelewa pia, hata kama atakiweka kwenye ubongo atakuwa amekariri tu na hili ndio tatizo tulilonalo hapa Tanzania.Ndio maana elimu yetu ni bora lakini haitoi maarifa ya kutosha kutuwezesha kupiga hatua mbele kiuchumi,kiteknolojia na kijamii.

Kama kiingereza kinaweza, kiswahili pia kinaweza, ingawa safari ya kukiwezesha ni ndefu na si rahisi!

Monday, September 17, 2007

Dk SLAA NI MFANO WA KUIGWA AUNGWE MKONO NA WATANZANIA WOTE!

Jana nilikuwa na usongo kweli wa kujua siku ya jumamosi ni watu gani ambao Dr Slaa aliwataja kama alivyoahidi,yaani wale wanaohusika na ubadhirifu wa fedha ya umma, kama ilivyo ada kwangu kwa siku za jumapili ninaelekea kanisani, kichwani nimepanga nikitoka tu nilisake gazeti lenye majina hayo. Nashawishika kununua gazeti la mwananchi lenye kichwa cha habari "Dk Slaa ataja vigogo wanaoitafuna nchi".Nilidhani ntayakuta majina mle ndani niwajue mafisadi hawa, wadau wa umasikini wa mtanzania azungukwaye na utajiri wa kila aina.

Kwa mshangao mkubwa sioni jina hata moja, zaidi ya kuona hawa waandishi wetu wa habari wanaandika,"miongoni mwa waliotajwa na Dk Slaa ni makatibu wakuu, wabunge wawili na mawaziri".Yaani kiujumla tu namna hiyo, halafu ndo imetoka.Hivi waliogopa nini kusema majina, mimi sijui taratibu za waandishi kwani hiyo si taaluma yangu, lakini wao si wangemnukuu tu Dk Slaa alichosema, tangu lini mjumbe akauwawa?

Kama na wewe hukuridhishwa na habari za vyombo vyetu vya habari siku ile basi tupia jicho pale kwa Mzee Mwanakijiji, amerusha hotuba ile msikilize na umsome kwa kubonyeza hapa.

Waandishi wa habari ni wakati sasa muanze kuthubutu kuwataja watu kwa majina jamii iwajue, hawa mafisadi ndio maadui wa uchumi wetu, hawa ndio maadui walioongezea wale kina ujinga, maradhi na umasikini, yaani amaadui hawa wametutengenezea adui aitwaye ufisadi au rushwa.Hawa wanapaswa kuchunguzwa na ikithibitika tuhuma zinazowakabili ni za kweli wafilisiwe na waukabili mkono wa sheria.

Hatuwezi kupiga hatua mbele kiuchumi kama tutaendelea kuwakumbatia hawa wezi, mafisadi wanaoitafuna nchi yetu,huku ndugu zetu wakikosa huduma bora za afya, elimu, maji safi, makazi bora nk

Tunataka kuona kuwa ile kauli mbiu ya maisha bora kwa kila mtanzania haikuwa danganya toto ya kupatia kula 'kura' bali ilikuwa na nia ya kweli ya kuboresha maisha ya mtanzania.

Takukuru nao wazifanyie kazi taarifa hizo, wawachunguize, kwani ni kazi yao.

Kitendo alichokifanya Dk Slaa ni cha kijasiri na cha kuungwa mkono na watanzania wote.

Tuamke sasa tupambane na maadui wa uchumi wetu.