Tuesday, December 2, 2008

TUWAKATAE VIONGOZI WACHAFU,WALAFI NA MAFISADI!!

Hakuna lisilowezekana katika sayari hii izungukayo!Kila jambo lina wakati wake, wakati hubadilika, binadamu hana budi kwenda na mabadiliko hayo vinginevyo atabaki nyuma na kuachwa na wakati.Kwa muda mrefu Afrika imefanywa kuwa nyuma kutokana na uongozi mbaya wa viongozi walafi wapenda madaraka, wenye utajiri wasioweza kuutolea maelezo, walioupata kutoka kwa kidogo kilichopaswa kuwafikia wananchi wao.

Kile kidogo ambacho kingeweza kuinua maisha ya wananchi wao wamekibinafsisha, ni mithili mfugaji mwenye kutamani kupata ongezeko la maziwa kwa ng'ombe wake bila ya kumuongezea lishe,kumtafutia majani mabichi, wametamani kukamua ng'ombe maziwa yote hata waone matone ya damu, na wametamani maziwa hata kwa ng'ombe dume!!!!

Afrika ambayo imepigania uhuru wake kuanzia miaka ya hamsini bado haijawa huru kiuchumi hata kifikra!!, wako wapi mashujaa wetu wa leo?

Wako wapi kina Julius Nyrere, Kwame Nkrumah, Samora Machel, Nelson Mandela wa leo?, ni lini walikoma kuzaliwa ndani ya Afrika viongozi mithili ya hao?, Bado tunashuhudia Afrika ikiliwa kwa nje na nchi tajiri na kwa ndani na viongozi walafi, hali ikiwepo kasi ndogo na sheria iliyolegezwa na nguvu ya pesa kuwazuia wailao kwa ndani pamoja na kukosa ujasiri wa kupambana na wale wailao kwa nje.

Mwalimu Nyerere wakati akizitetea nchi za dunia ya tatu, alipata kuwakemea mabepari, nchi tajiri,walipokuwa wakishinikiza tuwalipe madeni yao, hela waliiyotunyonya na kutukopesha, akawaambia ni sawa na kumtoa damu mgonjwa mahututi,Afrika iko mahututi kichumi bado!!, wazungu wale walimuelewa Mwalimu!!, Ni nani anayeendeleza mapambano hayo kwa kasi ile ile leo?

Leo tunaona jinsi siasa inavyokimbiliwa hata na wanataaluma, wanajua ni rahisi kuneemeka ukiwa huko,hasa kwa walio na dhamiri zilizokufa,wanaothubutu hata kuchota mapesa ya kununua madawa na kununua magari ya kifahari!!, wanasayansi wamekimbilia siasa, kwa staili hii maendeleo yakujaje?

Kuna ujasiri mwingi na thubutu kubwa ambayo viongozi wetu walio safi wanapaswa kutuonyesha, na wasipofanya hivyo, basi umma utawalazimisha kwani wakati wa mabadiliko ukifika hakuna awezaye kuuzuia, na atakayejaribu kufanya hivyo atakuwa anapambana na nguvu kubwa asiyoiweza!!

Hapa Tanzania tumeshuhudia mawaziri wawili Basil Mramba na Daniel Yona wakipandishwa kizimbani kujibu mashitaka ya jinsi walivyotuibia, tunahitaji mwendelezo wa mapambano haya dhidi ya wale wailao nchi nyetu kwa ndani kwani ni wengi na wasiopaswa kuongoza kwa wakati wa sasa!!

Tuwakatae kama Mwalimu alivyotuasa!!!

Tuko kwenye zama nyingine kabisa,, hakuna lisilowezeakana!!!!!