Friday, September 28, 2007

HOJA YA KUANZISHWA BLOGU YA WABUNGE NA WANANCHI!

Mara nyingi katika mijadala isiyo rasmi ninayoifanya na watu mbalimbali tunapojadili mambo ya siasa tunakubaliana kuwa tatizo kubwa la siasa ya nchini kwetu ni mfumo mzima unaoendesha siasa.Ni kama vile wananchi hatuna sauti na nguvu ya kuwaaambia wawakilishi wetu bungeni kuwa ni nini tunataka, na wao wakakisimamia kuhakikisha kinafanyika, kwa hali ilivyo sasa ni kama vile wabunge hatujawatuma wametumwa na chama hasa wale wa CCM.Wanasikiliza zaidi chama kuliko wananchi wanaowawakilisha.Mfumo huu haufai na tunaweza kuurekebisha.

Hivi kwa nini kusiwe na blogu, mfano www.wasiliananawabunge.blogspot.com, ambayo itawakutanisha wananchi na wabunge,kabla ya wabunge kwenda Dodoma na wakati wakiwa Dodoma tuwaeleze nini waihoji serikali kwa niaba yetu, na tusiporidhika wakiwa huko huko Dodoma tuwaeleze hatujaridhika na majibu ya Serikali ili wahoji, wahoji na wahoji hadi majibu yapatikane.Vinginevyo tutaendelea kusikia majibu ya porojo ya kila siku wanayojibu mawaziri wetu ,yasiyo na nguvu ya uwajibikaji, majibu kama, serikali iko mbioni kushughulikia swala x,serikali inafuatilia kwa karibu suala y,serikali ina mkakati wa kufanya swala z,serikali imejizatiti kuondoa uasikini ifikapo mwaka f,serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kero h inakwisha, majibu haya hayatoshi na yanahitaji maswali mengine zaidi lakini wabunge wetu huridhika nayo.

Wakati umefika sasa wa kuwa na jukwaa la kuwaambia wabunge wetu pale tunapotaka waihoji serikali na tusiporidhishwa na majibu ya serikali.

Blogu hii pia iwe na e mail address na namba za simu za wabunge wote.

Tutaendelea kuyanyoosha yaliyopinda, hadi pale yatakaponyooka.

Hoja hii ninaikabidhi jumuiya ya wanablogu Tanzania, JUMUWATA, ikifaa ifanyiwe kazi na isipofaa itupiliwe mbali.

Naomba kuwasilisha!

Thursday, September 27, 2007

WABADILIKE WATUTUMIKIE AU WAJIUZULU WAKALIME

Wakati tuliousubiri haukuwa mbali sana kama nilivyofikiri, wakati huo si tu kuwa umekaribia bali umefika.

Kila kilichofichwa kichakani kitawekwa juu milimani na kila kilichofichwa gizani kitawekwa kweupe nuruni, ili kila mwenye macho aone.Bonyeza hapa uone yale yaliyofichwa ambayo Dk Slaa ameyafichua, tunamshukuru Mwanakijiji kwa kutuwekea ripoti hii ya Dk Slaa.

Hatuwezi kuufumbia macho ubadhirifu unaotendwa na viongozi wetu,hawa mafisadi wanaoutenda na wajue sasa kwamba siku zao zinahesabika, kwa kuwa viongozi wao waliowateuwa wanawahifadhi na kuwaonea aibu kuwawajibisha sasa wananchi wanawaanika kweupe, wachague sasa kujiuzulu na kwenda kulima au kubadilika na kuwatumikia wanachi kwa uaminifu.

Wasidhani tumelala tunawaangalia kwa macho mawili.

KISWAHILI NA KIINGEREZA KIPI ZAIDI?

Bila shaka usomapo unajibu la swali hapo juu?, najiuliza tu.Waafrika tuna kaugonjwa fulani kakudharau cha kwetu. Ndio.Yawezekana ni athari za ukoloni, waliviita vya kwetu vya kishenzi nasi tukaviona hivyo na kuvitukuza vya kwao na hii iko hadi leo.
Hii imepelekea kuiga kila cha mzungu, angalia leo utamaduni wetu ulivyopindapinda, haueleweki,sijui ni nini utambulisho wa mtanzania wa leo.Mimi nadhani ni Kiswahili chake tu!

Angalia dada zetu vivazi vyao, kuna wakati kulikuwa na uvumi kuwa presidenti wetu kapiga marufuku aina fulani ya vivazi vya dada zetu,wao wanaita vya kizungu,wengine waita vya kihuni!, jamaa wakazua kuwa mgambo watatanda na bakora halafu aonekane binti na kivazi cha kutatiza,analamba viboko kadhaa kama adhabu na onyo.Siku moja waandishi wa habari wakapata upenyo wakamuuliza mkuu, akajibu hana mpango wa kuchukua hatua hiyo, hayo ni mambo ya fashion tu, yatapita kama zilivyopita suruali za chini nimwagie miaka ileeeeeeeee. Vijana wa kiume wa kileo nao wamekuwa wazungu, wanasuka nywele, suruali zinavaliwa chini ya matako, ati mambo ya kizungu!.Mambo ya kuiga hayo!
Ni kwa vipi tutaweza kuulinda utamaduni wetu ulioingiliwa na utandawazi?

Leo hii tunaona kiingereza ni bora kuliko Kiswahili, tunaona hakifai kutumika kama lugha ya kufundishia, kama lugha inayofaa kutumika maofisini.Je tatizo hili ni la lugha au wenye lugha?.Si kuwa lugha ya kiswahili haiwezi kubeba kazi hizi, wenye lugha wameidharau lugha yao wamekitukuza kiingereza zaidi.Yawezekana kuwa lugha hii ina mapungufu lakini upungufu huu hauhalalishi kutokufaa kwa lugha hii, upungufu huu ni changamoto kwa wataalamu wetu wa kiswahili waweze kukiwezesha kiswahili kujitosheleza kutumika, mitaani kuwasiliana, mashuleni kufundishia, maofisini kwa mawasiliano ya kikazi.Wataalamu wetu watafsiri kwa kiswahili fasaha kila kilicho kwa kiingereza kiandikwe kwa kiswahili, kila kitu, vitabu vya mashuleni,maofisini,sheria zitumikazo mahakamani, vitabu vya maelekezo kwa wakulima juu ya matumizi ya mbolea na umwagiliaji,mikataba yote nchi hii inayoingia itafsiriwe pia ili wale wasio ijua lugha ya kiingereza waelewe yaliyoandikwa.

Kuna mwalimu wangu mmoja alinifundisha hesabu, tuition, enzi hizoooooooooooo, alijulikana kwa jina la ‘Mr So Much’, anasagia kwelikweli kiswahili anasema hakifai, anatupa mfano, anasema, kama kiswahili kingetumika kufundishia ingekuwa taaaabu kwelikweli, anatoa mfano, hapo anafundisha topic ya calculus, differentiation, sentensi kama ‘we differentiate y with respect to x’,dy/dx, tungesema ‘tunanyambulisha x kwa heshima ya y’, hapo hoja yake inakuwa kiswahili hakitoshi kufundishia na anatushawishi.Kwa wakati ule alitushawishi wengi tukakubali kuwa kiswahili hakifai kufundishia.Nadhani kina mapungufu yanayohitaji kurekebishwa na kuboreshwa.

Ukweli ulio wazi ni kwamba kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kuelewa masomo yao darasani na kufaulu usahili wanapoomba ajira.Endapo Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia kitamuwezesha mwanafunzi kuyapokea maarifa anayopewa na mwalimu wake kwa urahisi zaidi, ilivyo sasa mwanafunzi inabidi amsikilize mwalimu, atafsiri kinachofundishwa kutoka kiingereza kwenda kiswahili,akifanyie kazi akilini na kukihifadhi kwenye ubongo.Akishindwa kutafsiri alichosikia atashindwa kuelewa pia, hata kama atakiweka kwenye ubongo atakuwa amekariri tu na hili ndio tatizo tulilonalo hapa Tanzania.Ndio maana elimu yetu ni bora lakini haitoi maarifa ya kutosha kutuwezesha kupiga hatua mbele kiuchumi,kiteknolojia na kijamii.

Kama kiingereza kinaweza, kiswahili pia kinaweza, ingawa safari ya kukiwezesha ni ndefu na si rahisi!

Monday, September 17, 2007

Dk SLAA NI MFANO WA KUIGWA AUNGWE MKONO NA WATANZANIA WOTE!

Jana nilikuwa na usongo kweli wa kujua siku ya jumamosi ni watu gani ambao Dr Slaa aliwataja kama alivyoahidi,yaani wale wanaohusika na ubadhirifu wa fedha ya umma, kama ilivyo ada kwangu kwa siku za jumapili ninaelekea kanisani, kichwani nimepanga nikitoka tu nilisake gazeti lenye majina hayo. Nashawishika kununua gazeti la mwananchi lenye kichwa cha habari "Dk Slaa ataja vigogo wanaoitafuna nchi".Nilidhani ntayakuta majina mle ndani niwajue mafisadi hawa, wadau wa umasikini wa mtanzania azungukwaye na utajiri wa kila aina.

Kwa mshangao mkubwa sioni jina hata moja, zaidi ya kuona hawa waandishi wetu wa habari wanaandika,"miongoni mwa waliotajwa na Dk Slaa ni makatibu wakuu, wabunge wawili na mawaziri".Yaani kiujumla tu namna hiyo, halafu ndo imetoka.Hivi waliogopa nini kusema majina, mimi sijui taratibu za waandishi kwani hiyo si taaluma yangu, lakini wao si wangemnukuu tu Dk Slaa alichosema, tangu lini mjumbe akauwawa?

Kama na wewe hukuridhishwa na habari za vyombo vyetu vya habari siku ile basi tupia jicho pale kwa Mzee Mwanakijiji, amerusha hotuba ile msikilize na umsome kwa kubonyeza hapa.

Waandishi wa habari ni wakati sasa muanze kuthubutu kuwataja watu kwa majina jamii iwajue, hawa mafisadi ndio maadui wa uchumi wetu, hawa ndio maadui walioongezea wale kina ujinga, maradhi na umasikini, yaani amaadui hawa wametutengenezea adui aitwaye ufisadi au rushwa.Hawa wanapaswa kuchunguzwa na ikithibitika tuhuma zinazowakabili ni za kweli wafilisiwe na waukabili mkono wa sheria.

Hatuwezi kupiga hatua mbele kiuchumi kama tutaendelea kuwakumbatia hawa wezi, mafisadi wanaoitafuna nchi yetu,huku ndugu zetu wakikosa huduma bora za afya, elimu, maji safi, makazi bora nk

Tunataka kuona kuwa ile kauli mbiu ya maisha bora kwa kila mtanzania haikuwa danganya toto ya kupatia kula 'kura' bali ilikuwa na nia ya kweli ya kuboresha maisha ya mtanzania.

Takukuru nao wazifanyie kazi taarifa hizo, wawachunguize, kwani ni kazi yao.

Kitendo alichokifanya Dk Slaa ni cha kijasiri na cha kuungwa mkono na watanzania wote.

Tuamke sasa tupambane na maadui wa uchumi wetu.

Tuesday, September 11, 2007

SEPTEMBER 11

Tarehe hii ya leo mawka 2001 itabaki kuwa ya kukumbukwa, ni siku ambayo dunia ilishuhudia unyama na ukatili wa hali ya juu.Ni tukio la kigaidi lililoitikisa dunia. Angalia picha hii ujionee tukio hili la kikatili na kwa habari zaidi angalia hapa.

Friday, September 7, 2007

KILA LA KHERI TAIFA STARS


Kesho wawakilishi wetu, Taifa Stars wanachuana na Msumbiji ndani ya uwanja mpya.

Tuna njaa, kiu na shauku ya ushindi, tunataka kuiona timu yetu ikitoka uwanjani na ushindi na tuna kila sababu ya kushinda katika uwanja wetu wa nyumbani.

Taifa Stars oyeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeee!

Mungu ibariki Taifa Stars!

Mungu ibariki Tanzania!