Sunday, July 29, 2007

TUNAHITAJI MABADILIKO

Mabadiliko ya kweli hutoka chini kwenda juu,binadamu ni mwepesi wa kusahau alikotoka,pale anaposhiba humsahau mwenye njaa, ndivyo ilivyo kwa viongozi wetu hawaguswi na matatizo yetu raia tuliowachagua, watarudi kwetu kuomba kura 2010. Ndani ya Serikali wanalindana,hakuna anayewajibishwa, ndani ya bunge wanatetea maslahi ya chama badala ya maslahi ya taifa na watu wake. Ndani ya mahakama nako kunanuka rushwa, pale ambapo tunategemea kuipata haki, sheria hulegezwa na pesa!. Ukikwama unaambiwa nyoosha mkono mambo yatakaa sawa.Kwa mwendo huu hatufiki kokote. Ni lazima tubadilike. Mambo haya mengi yaliyooza ndani ya mihimili yote mitatu ni matokeo ya mfumo mbovu, ndio maana iko haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa wa kuyaangalia mambo haya kwa undani, ndiyo maana iko haja ya kuibadili katiba yetu tuupange sawa mfumo mzima wa mihimili ya dola.Kutokufanya hivi ni kuuendeleza uozo kwa vizazi vijavyo.Kama tunasema Serikali hii ni ya watu iliyowekwa na watu kwa ajili ya watu ni kwa nini ione kigugumizi cha kutunga katiba mpya.Bila kumung'unya maneno, katiba iliyopo sasa haifai, no checks and balance!

Iweje leo watu waliotukosea kama taifa kwa kusaini mikataba mibovu huku wakila ten percent waendelee kukalia ofisi zao?,Mwalimu aliwainisha maadui watatu wa maendeleo yaani ujinga, umasikini na maradhi sasa tuuongeze na ufisadi. Kiongozi asiyeweza kupambana na ufisadi hafai tumkatae.Wamesaini mikataba ya Richmond,ATCL,IPTL na mingine.Je hawa si wezi wanaotakiwa kushughulikiwa?Mimi hujiuliza nini maana ya kumchoma moto mwizi anayeiba kuku mtaani na kumuacha huyu fisadi na mwizi anayetuibia mabilioni?,siungi mkono kuchoma wezi moto, ninachohoji ni kwa nini hatuoni ulazima wa kuwataka hawa wala rushwa wapishe viti
na kuukabili mkono wa sheria?

Raisi Kikwete aliwahi kutueleza kuwa anawajua wala rushwa kwa majina akawapa muda wajirekebishe.Kwa kuwa hawajajirekebisha, anangoja nini kuwatimua?, Hii ni alama gani kwa utawala wake?

Wauza dawa za kulevya majina yao tuliambiwa yamekabidhiwa kwa vyombo vinavyohusika.Hadi leo kimya! Mimi sielewi. Huu ni uozo mwingine.Nani anayepiga kelele tena juu ya biashara hii chafu baada ya sauti ya shujaa Amina Chifupa kunyamazishwa na kifo?, nitajieni jina la mbunge mmoja tu aliyeanza kumuenzi Amina kwa kuendeleza mapambano dhidi ya madawa ya kulevya.Haya madawa yanateketeza vijana wetu, Amina alilitambua hili akalishikia bango, sasa Amina hayupo, ni nani anayesema aluta kontinua?

Leo hii kuna vijana wa Tanzania wapatao 24 ambao Serikali imewakana kule Ukraine.Imesema walienda kwa njia zao wenyewe na serikali haiopo tayari kuwapa mkopo waendelee na masoma yao.Mimi najiuliza hivi hata kama wamekosea si wangeelezwa tu waombe radhi kwa barua kukiri kosa na kuendelea na masomo yao?Hivi kosa lao la sasa si ni faida ya taifa kwa baadae?Au wasomi tulionao leo wanatosha?Je ni nani asiyejua kuwa elimu ya nchi za nje huko ughaibuni ni bora kuliko ya kwetu hasa kwa kuwa wao wameendelea kisayansi na kiteknolojia kuliko sisi? Serikali isiniambie kuwa haina hela, ninajua kuwa zipo na zinatumika vibaya bila ya kuwajibishana achilia mbali magari ya kifahari wanayotembelea viongozi wetu. Hembu wanieleze waliotumia vibaya fedha ya serikali kama ilivyoonyeshwa katika ripoti ya Chief Auditor General wamefanywa nini?,hii hela iliyopotea ingeweza kuwalipia hawa vijana kule Ukraine na chenji ikabaki ya kuwalipia na wengine.Huu nao ni uozo mwingine.Wabunge wetu wameshindwa kuwatetea kwa kuwa wanawakilisha chama bungeni, wale wa upinzani walijaribu kwa nguvu zote kuwatetea lakini sauti zao bado ni ndogo kwa kuwa idadi yao ni dogo, ujumbe tunaoupata sisi raia ni kwamba tuiogeze idadi ya wabunge wa kambi ya upinzani bungeni wakatutetee.Pamoja na wabunge kushindwa umma wa watanzania nao umeshindwa kuwaokoa wale vijana japo hata kwa maandamano ya amani, hapo ndipo viongozi wetu wanaona watanzania ni watu poa sana, hawana noma kabisa. Bila shaka raia wa nchi hii ni wapole kuliko raia wote duniani, upole wa kusikia kukubali na kutopinga jambo lolote hata kama lina madhara kwetu. Tusipobadilika majirani zetu , Kenya na Uganda wataendelea kutudharau.Eti tuna amani na utulivu!, mimi si ukubali upuuzi huu,kilichopo ni woga na uzuzu!

Tutakuwa na amani na utulivu tutakapokuwa na Serikali inayosikiliza shida za watu na kuzitatua, inayopambana na wala rushwa wakubwa na wadogo, inayowajali masikini,inayowawajibisha watumishi wake wanapokosea,inayotoa haki kwa wote bila kujali nguvu ya pesa,inayotumia mali asili yake kwa manufaa ya raia wake,inayotoa elimu bora kwa watu wake.
Tunakuwaje na amani na utulivu wakati tunaibiwa na viongozi mabilioni kwa kutia saini mikataba yenye utata?, mimi sielewi!

Bunge nalo sijui kwa nini limegeuka kituko, ni bunge la aina yake duniani!. Ukweli huwa mbaya ukiangaliwa vibaya.Nikisema kituko sitanii. Hembu fikiria mbunge anaongea anpinga zaidi ya asilimia sabini na tano ya hoja fulani ya Serikali au bajeti ya wizara fulani halafu mwishoni anasema "mheshimiwa spika naunga mkono hoja".Mimi sielewi.Naona usanii mtupu.Ile speed and standard imegota sawa tu na ile ari, nguvu na kasi ambayo tuliambiwa kuwa sasa zingekuwa mpya.

Ni mara mbili nimewasikia wabunge wakimpongeza raisi Kikwete,si vibaya kumpongeza.

Mara ya kwanza walimpongeza kwa kuiilaani filamu iliyotengenezwa na Hubert Sauper ya Darwin’s Nightmare ijulikanayo kama Filamu ya mapanki kwa kuwa imeidhalilisha nchi yetu.Hoja hii iliwasilishwa na mbunge Mudhihir Mudhihir iliungwa mkono ikachangiwa kwa kishindo!
Kwa kuwa raisi alisema atashugulukia mikataba sasa wamuunge mkono kwa hili pia, wawasilishe hoja ya kuwalaani wale wote walioiigiza nchi yetu kwenye mikataba mibovu na wala rushwa wote.Hawa ndio maadui wa maendeleo yetu.

Mbunge wa Ukerewe Getrude Mongela akawasilisha hoja, eti anampongeza raisi kwa kuwaita watendaji wa serikali na kujadili ripoti ya Chief Auditor General.Ripoti ilionyesha wajanja wamekula hela.Wamempongeza raisi kwa lipi?, si alikuwa anatimiza wajibu wake?Je ni wezi wangapi katika hao waliohusika kama ilivyoonyeshwa ndani ya ripoti hiyo wamechukuliwa hatua?,ningeiona mantiki ya kumpongeza kama angewafukuza kazi wote walioiba fedha ya serikali.

Wabunge hawa wameiacha bajeti inayomkandmiza mtu duni ipite, siku ya kwanza ya machungu ya bajeti hii ni pale nauli zilipopanda, za mikoani kisha za daladala jijini Dar es salaam.

Naongea na kijana mmoja ndani ya daladala tarehe 25 July 2007 siku ya kwanza nauli ya daladala kupanda jijini Dar es salaam:

Ananiambia "Sijui itakuwaje maisha yanapanda mishahara iko pale pale, kwa nini wasiangalie
sekta binafsi, mishahara yetu midogo sana"

Namuuliza "Kwani unatokea wapi?"

Anajibu " Magomeni napanda hadi Drivin kisha natembea hadi macho pale CCBRT ,ni mwendo
wa kama dakika kumi hivi, halafu napanda gari la Masaki"

Namuulza "Kwani unalipwa shilingi ngapi?"

Anajibu " Ni elfu arobaini na nae, miezi mingine wanatoa nauli inaongezeka inafika elfu 60"

Jamaa anatumia elfu thalathini na tatu kwa mwezi nauli tu,anabakiwa na elfu kumi na tano!, Ni sauti gani ya utetezi inayotoka kwa mbunge anayemuwakilisha kijana huyu?Haya ndio mambo ya kupigia kelele bungeni, hadi kieleweke!, ukweli ni kwamba wafanyakazi wengi wananyonywa, hapa ninaongelea sekta binafsi.Hivyo unyonyaji bado ungalipo.Nani anawatetea hawa bungeni?

Umefika wakati sasa raisi Kikwete afahamu kuwa tunataka kuiona nchi inasonga mbele. Kwa sasa imegota.

Umefika wakati wabunge wetu wafahamu kuwa hatukuwatuma kuwakilisha chama na kulinda maslahi ya chama chao.Tumewatuma kulinda maslahi yetu na taifa letu, wakishindwa hawastahili kuendelea na kazi. Wasidhani tumelala,tuko macho tunawaangalia wanavyoitenda kazi tuliyowatuma, ambayo kwa sasa utendaji wao ni duni mno.

Wateteeni watu wetu.

Ondoeni unyonge wa watu wetu dhidi ya waonezi wetu.

Pambaneni na ufisadi unaowazunguka watu wetu.

Huu ni wajibu wenu, muutimize.

Tunahitaji mabadiliko.

Monday, July 9, 2007

Kauli ya Katibu Mkuu Umoja wa Mataifa,Ban Ki-Moon

“Mazoea yangu kila siku asubuhi huenda hayatofautiani na yako. Tunachukua magazeti na kufungua television,iwe mjini New York,Lagos au Jakarta kuangalia mateso ya kila siku yanayomkabili binadamu.Inawezekana kuwaDarfur,Lebanon au Somalia”

Anaendelea …………………………. na kumalizia,

“Kila asubuhi tunaweza kusoma kwenye magazeti. Lakini ni kwa jinsi gani tunasikiliza sauti za watu hao au kujaribu kwa nguvu zote na kwa kudhamiria kuwasaidia?Nawaomba mfanye hivyo”

Hii ni kauli nzito inayotoka kwenye hisia kali za kiongozi anayewajali watu anayewaelekeza viongozi kuwa watumishi wa watu.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon anachojaribu kuwaeleza viongozi hawa ni kuwa haya mateso tunayoyaona kwenye runinga, tunayoyasoma kwenye magazeti na tunayoyasikia kwenye radio wasiyapuuze, wasiyaangalie tu, wasiyasome tu.Wayatatue kwa nguvu zao zote.

Ni kama vile anawaambia huu ni wajibu wenu muutekeleze.

Ni kama vile anawaambia mshikwe na huruma mnapoona na kusoma matatizo yanayowazunguka watu wenu na kuutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.

Ni kama vile anawaambia msiidharau sauti ya watu inapobeba kero zao na kuzileta kwenu, zitatueni kero zao.

Ni viongozi wanagpi tulionao hapa Tanzania wanaolitekeleza ombi hilo la Katibu mkuu kwa vitendo?,Wananchi wengi ukiwsaikiliza wamechoka, wamepoteza matumaini kwa viongozi waliowachagua. Hakuna anayemjali mskini.Koti la umaskini wa watu wamelitupa, watalivaa tena wakati wauchaguzi ukiwadia. Ndio nchi hii ilipofikia.Watanganyika sasa wanaitwa Wadanganyika!.Tunadanganywa na viongozi miaka mitano mitano!

Hivi yale maisha bora kwa kila mtanzania tuliyoambiwa yako wapi?

Kwa mujibu wa nukuu ya Ban Ki-Moon hapo juu, ni kiongozi gani, ni mbunge gani anayeweza kunyoosha kidole akasimama akatueleza namna anavyotumia mudawake kutatua kero za watu anaowaongoza?. Unatoka wapi uhalali wa viongozi butu kama hawa kuendelea kuongoza?. Mbona hawazisikii sauti za watu na kuwasaidia?

Wa kale walisema “sauti ya watu ni sauti ya Mungu”,mbona wameikana busara hii ya wazee wetu wa zamani?

Kuna ufisadi mwingi unaotuzunguka, kuuacha upite nakuendelea kwenye kizazi kijacho ni kutokitendea haki kizazi hicho cha wana wetu na wana wa wana wetu.Ni kutokuwajibika.Iwe kwa mijadala au njia yoyote ile tunahitaji mabadiliko!Mbona tuliupigania uhuru, lakini matunda yake tumeyaacha yawafaidishe wajanja wachache?Hakika kizazi hiki kina jukumu kubwa la kufanya kuuondoa uozo uliopo.Mafisadi hawa wameingia mikataba mibovu kwa maslahi yao. Bado wengine wangali wakikalia viti vyao.Kwa nini?

Yule mkuu wa Benki ya dunia alipopata kashfa ya kumpandisha cheo mpenzi wake na kumuongezea mshahara,sasa amewekwa pembeni.Mbona hapa kwetu huyu mkuu wa benki kuu ana tuhuma za ulaji anaendelea kukalia kiti? Si inasemekana anatarajiwa kuchunguzwa?.Taifa hili linahitaji muelekeo mpya. Linahitaji kuwa na utaratibu wa kuwatambua wenye maadili wanaofaa kuongoza lakini pia kuwe na utarataratibu wa kuwachukulia hatua kali wanaokwenda kinyume na taratibu hizo bila kulindana.

Viongozi wetu watekeleze wito wa katibu mkuu, Ban Ki-Moon.

Mungu ibariki Tanzania,

Mungu ibariki Afrika.