Wednesday, October 24, 2007

GAZETI JIPYA RAIA MWEMA!

Moja ya magazeti ambayo nilitokea kuyapenda kwa muda mrefu sana ni gazeti la Rai.Hii ilitokana na umakini na ujasiri wa waandishi wa gazeti hili.Ninaamini kabisa kuwa magazeti yana sehemu kubwa katika kujenga fikra zetu, kutufundisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutuonyesha uozo, au tuuite ufisadi, ndani ya jamii yetu na hata namna ya kupambana na uozo huo. Magazeti yakiandika habari za kweli na kwa uwazi yataweza kuisaidia jamii yetu kusonga mbele kifikra na kimaendeleo.

Nakiri kwa kusema kuwa hamu ya kulisoma gazeti la Rai imenitoka,siku hizi nalinunua kwa mazoea tu, umakini na uandishi wa gazeti hili sio ule wa walipokuwa wakiandika akina Jenerali Ulimwengu na Maggid Mjengwa.Nadhani sasa gazeti hili jipya la “Raia Mwema” litaziba pengo lililoanza kujitokez andani ya Rai, sijui gazeti la Rai limekumbwa na nini.Sielewi!

Muda mfupi nimeisoma habari ya kuanzishwa kwa gazeti hili, na wiki ijayo inatoa toleo la kwanza, miongoni mwa waandishi ni Jenarali Ulimwengu, Prof Issa Shivji,Maggid Mjengwa, Mihangwa na Padri Pivatus Karugendo.Kama unawafahamu waandishi hawa basi usikose kusoma makala zao!.Utaniambia mwenyewe!

Sina shaka na hawa waandishi kuwa kuwa wamekubuhu katika taaluma ya uandishi wa habari, watakuwa na ujasiri wa uandika yale ambayo wengine wameogopa, watashiriki katika mchakato wa kuisafisha jamii yetu inayoendelea kuchafuliwa na ufisadi, utandawizi na mmong’onyoko wa maadili.

Kila la kheri gazeti la “RAIA MWEMA” ninaahidi kukunua kila utokapo!

Sunday, October 21, 2007

WATU WAOVU WAMEMUUA LUCKY DUBE!

Ni mchana wa ijumaa niko sehemu napata msosi wa mchana, pembeni jamaa anaongea na mwenzake, Lucky Dube amefariki, nayasikia maongezi yale, kwa kuwa sikuwa mbali na meza yao.Nashangaa!.Namuuliza mmoja wao , ananiambia ni kweli jamaa wamemuua Lucky Dube.Jioni siku hiyo hiyo ya ijumaa nasikiliza Voice of America, nasikia wanatangaza kuwa Lucky Dube ameuwawa.

Nikiwa njiani nakutana na ajali daladala,DCM, imeuvaa mti, mtu mmoja amefariki, mwili wake ukiwa bado umelala barabarani!
Maisha ni safari yenye mwisho,hakuna ajuaye mwisho huu unafika lini!,Lucky Dube hakujua kama siku ile angeaga dunia,watu wasio na utu wamemuua, ni watu wenye dhamiri zilizokufa tu, ndio wawezao kufanya kitendo cha kinyama kiasi hicho!

Kijana yule angejua kuwa gari lile lingepata ajali asingalipanda daladala lile!,kifo ni kitu ambacho tumefichwa tusijue kinakuja lini na kwa staili gani!
Anyaway, maisha hayana budi kuendelea!

Ni aina ya uaimbaji wake na ujumbe ndani nyibo zake ndizo zinisukumazo kuandika juu yake.South Afrika na Afrika kwa ujumla imempoteza
mpambanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi,mwanamapinduzi na mpigania haki za watu wanyonge Lucky Dube!

He has gone but the messages in his songs will continue to live!

Sunday, October 14, 2007

NYERERE DAY

Ninaikumbuka siku hii ya leo, miaka 8 iliyopita, tarehe 14 october 1999,nikiwa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha Dar es salaam, kitivo cha uhandisi, nakumbuka tulikwa kwenye kipindi katika karakana ya umeme. Mara tukasikia wimbo wa taifa unapigwa,kila mmoja anaikimbilia radio kisha tunamsikia raisi wa awamu ya tatu,Mkapa anatangaza Mwalimu Nyerere amefariki dunia! Baada ya muda uongozi wa chuo unatoa tangazo la kusimamisha ratiba zote za vipindi.Ilikuwa mshtuko mkubwa.Baada ya siku kadhaa mwili unawasili Tanzania chuo kikapanga utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanachuo kwenda kuuaga mwili wa hayati Mwalimu Nyerere,nilikuwa mmoja wa waliofika uwanja wa taifa kuuaga mwili wa Mwalimu, usiku wa manane lakini ilikuwa kama mchana jinsi watu walivyojaa.Umati ule unanifundisha jambo moja 'kuongoza ni kujitoa kwa ajili ya unaowaongoza', Mwalimu aliyatoa maisha yake kwa ajili ya taifa lake, aliishi alichokisema na alisema alichokiishi tofauti na viongozi wetu wa leo!

Tunapoikumbuka siku ya kufariki kwa Mwalimu Nyerere hii leo tujiulize maswali yafuatayo:-

Hivi mwalimu angalikuwepo soo kama la Richmond Development Cooperation lingepita kimizengwe vile na mambo yakaisha kiaina kama yalivyoisha?
Sasa tunaambiwa kuwa mkataba ule ulisainiwa usiku na Tanesco hawajui ni nani aliyeusaini. Inashangaza!

Hivi ule mkataba tata wa madini wa Buzwagi ungepita hivihivi bila kuundiwa tume huru aliyoiomba Mbunge Zitto?
Bila shaka Mwalimu angemwagia sifa Zitto Kabwe hadharani na kuwasuta wabunge wa CCM waliomfukuza bungeni.Bila shaka angesema kuna haja ya waziri Karamagi ajiuzulu!

Hivi ile kashfa ya ufisadi aliyoiibua Dk Slaa, wale waliotajwa angelipuuziwa kama ambavyo wanafunzi wake wamepuuzia? Bila shaka angaliwaita wote Butiama na kuwahoji maswali magumu, na labda angalishauri baadhi yao wajiuzulu!

Hivi Mwalimu angalikuwepo wanafunzi Mlimani wangelipishwa 40% ya ada? Bila shaka angalikemea kwa nguvu zote!

Huyu ndiye Mwalimi ambaye miaka nane sasa bila yeye viongozi wetu wameshindwa kuweka dhamira yao kwa dhati na kwa vitendo kupambana na ufisadi, kwani hata ndani ya chanma alichokiasisi yeye Mwalimu nguvu ya pesa inatumika kupata uongozi!

Miaka minane bila Mwalimu Nyerere ujumbe kwa viongozi wetu ni kuwa, wamuenzi Mwalimu kwa vitendo na si kwa maneno kama wafanyavyo sasa,tumechoshwa na porojo, tumeschoshwa na maneno tunataka vitendo.