Wednesday, June 27, 2007

BURIANI AMINA

Ni asubuhi, naamka na ninaingia mtaani katika pilikapilika zangu za kawaida, njiani naona gazeti lenye kichwa cha habari Amina hatunaye tena. Nashangaa!. Namuita muuza gazeti na kununua gazeti kupata undani wa kilichoandikwa.Baada ya kusoma nathibitisha kuwa Amina Chifupa ameaga dunia. Hatunaye tena.

Kweli chema hakidumu!

Mithili ya Amina Chifupa ndani ya CCM sijamuona. Mfanao wa mpambanaji jasiri dhidi ya ufisadi miongoni mwa wa wabunge wa chama kinachotawala ukimuondoa Amina mwingine simjui.

Nikiwa nimepigwa butwaa, nachukua simu yangu ya mkononi, kufungua blogu ya ndugu Michuzi nakutana na habari inayoeleza kifo cha Amina Chifupa, ikieleza kuwa Amina amefariki usiku wa kuamkia jana saa tatu kasorobo katika hospitali ya jeshi Lugalo alikokuwa amelazwa.

Kweli duniani tu wapitaji. Mungu aipe nguvu familia ya hayati Amina Chifupa kustahimili katika kipindi hiki kigumu.

Ningeweza kuishia kutoa pole kwa familia,nikamaliza. Lakini kuna mengi ya kusema juu yake, kwa kuwa alikuwa akifanya kile ambacho watanzania tulipenda kumuona akiendelea kufanya. Kupambana na ufisadi unaotuzunguka. Tunakumbuka jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya madawa ya kulevya. Amina alithubutu kufanya yale ambayo wengi hawana ujasiri wa kuyafanya,kuiondoa hali ya hewa chafu inayotuzingira, alikataa kuiona harufu hiyo chafu kama hali ya kawaida.Alikemea, alihoji na alisimamama kwenye haki.Alikuwa mtetezi wa watu duni.Watu wa aina hii si wengi miongoni mwa viongozi wetu wa leo.Ni kweli kuwa ameacha pengo kubwa, ndani ya chama alichokuwapo, sijamuona wa kuliziba.

Binadamu tu wasafiri, maisha yetu duniani ni mafupi, na tuishi kwa kutende mema kwa jamii ituzungukayo, walio katika nafasi za uongozi na wawapende na kutenda haki kwa wale wanaowaongoza ili siku ya kuondoka itakapowadia matendo yetu mema yaendelee kuishi na jamii tuliyoiacha.

Wote tuseme mapambano yanaendelea.

Kwa heri mpendwa wetu

1 comment:

Anonymous said...

Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana libarikiwe.
Natoa pole kwa familia ya Chifupa