Sunday, August 19, 2007

MKATABA WA MADINI WA BUZWAGI ULISAINIWA CHURCHIL HOTEL UINGEREZA!

Mvua kubwa inanyesha, watu hawabanduki,mi nimejibanza kwenye mwamvuli wa jamaa nimekutana naye pale, kanihifadhi, ikitulia wanaume wanavua mashati wanakamua maji wanayavaa mashati yao tena, wana usongo kweli kweli wana hamu ya kumpongeza na kumsikiliza mbunge Zitto Kabwe ambaye hivi karibuni wabunge wa CCM wamememhukumu kwa kulidanganya bunge na hivyo kupewa adhabu ya kumzuia kuhudhuria vikao vya bunge hadi januari mwakani.

Mbunge Zitto kakaribishwa kuzungumza, kutokana na mvua iliyokuwa inanyesha waongeaji waliomtangulia walikuwa wakitumia mwamvuli, Zitto alivyoingia, akauliza,”kuna umuhimu wa kutumia mwamvuli?”, akaomba waondoe mwamvuli, akahutubia huku mvua inamnyeshea sawa na wale wanaomsikiliza.

Zitto kaongea mambo mengi makubwa yanayoonyesha uozo ndani ya mfumo uliopo unaokwamisha rasilimali zetu kulinufaisha taifa.

Kabla hajaanza kuhutubia, anawaomba wananchi wasimame na kuimba wimbo wa Tanzania Tanzanai. Nakupenda kwa moyo wote …………………………

Kuonyesha dhamira ya kuujenga upya uzalendo wetu uliopotea na wasio nao wabunge wetu wa chama tawala kwa kutanguliza maslahi ya matumbo yao na chama chao.

Anatuambia mwalimu wangu nje ya darasani, prof Issa Shivji aliniambia” Doubt everything” akiwa na maana “tilia shaka kila kitu”.Baada ya kutilia mashaka mkataba wa Buzwagi ndio maana akaamua kwa kushirikiana na wabunge wenzake wa upinzani kuwasilisha hoja binafsi ya kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza mapitio ya mikataba ya madini na mazingira ya kusainiwa mkataba mpya wa madini wa Buzwagi.

Akiongelea mkataba uliosainiwa anasema, namnukuu,”Mkataba ulisainiwa Churchil Hotel London, kwa kuwa mkataba huu ulisainiwa Uingereza ulipaswa kusainiwa kwenye ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza, ubalozi wa nchi ni nchi”.

Hili la mkataba kusainiwa hotelini linashangaza, na lilituacha wasikilizaji midomo wazi!

Waziri Karamagi alipaswa kutueleza ilikuwaje, na bado anapaswa kutueleza ilikuwaje akaacha kwenda kwenye ubalozi wetu kuifanya kazi hii akaenda hotelini?

Cha ajabu tumeambiwa, mkataba wa Buzwagi umesainiwa rais akiwa hajui,hapa napo sielewi!

Serikali ilisimamisha kusainiwa mikataba mipya hadi mikataba ya zamani ipitiwe upya ili iweze kulinufaisha taifa, hili alilisema rais mwenyewe.

Swali lilozuka ni kwamba ni kwa nini mkataba huu usainiwe tena kwa vigezo vya zamani ambavyo vina mapungufu mengi, yanayopfanya tusinufaike na madini yetu.Hapa kuna maswalia mbayo waziri Karamagia anapaswa atujibu kiufasaha.

Bila shaka CCM hawakujua kuwa kwa kumtimua Zitto wanajitafutia ubaya na umma wa watanzania!, bila shaka sasa wanajuta!.

Ni watu kama Zitto ndio watakaoleta mabadikliko.

Aina ya watu watetezi na wapambanaji kama Zitto ndio wananchi wa nchi hii wanaowahitaji!

Kwa yoyote aliyekuwepo kwenye mkutano ule jambo moja lilikuwa wazi ni kwamba wananchi wamechoka, hawaoni wanaozipigania haki zao na kuwatetea ndani ya serikali iliyopo, hakuna mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi.Sasa wanataka mabadiliko. Watu kama Zitto ndio wanaonekana wakombozi.

Sasa tunaikumbusha serikali hii yale yaliyosemwa katika Azimio la Arusha,

“Tumeonewa kiasi kutosha,tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Ni unyonge wetu ambao umefanya tuonewe, tunyonywe na tupuuzwe.Sasa tunataka mapinduzi kuondoa unyonge wetu, ili tusinyonywe tena,tusionewe tena na tusinyanyaswe tena”.

Haiwezekani na hatukubali kuendelea kuwa taifa la waoga, mazuzu na mandondocha, kwani woga wetu ndio mtaji wa mafisadi . Mafisadi hawa husema, “watanzania wanasema mchana, usiku wanalala wakaimka wameshasahau”,sasa tunawajulisha tu kuwa, siku zao zinahesabiwa, waache ufisadi tulijenge taifa letu.Wabunge wa CCM mpo hapo?

Hembu watanzania tulivae koti la ujasiri na tupambane na mafisadi.

Nanukuu kama alivyosema Mrema leo” Heri kuishi kama Simba siku moja kuliko kuishi kama inzi siku mia moja”

Dk Slaa “Mwizi ntakufa nae”

Free Mbowe “ Haki haiombwi , hudaiwa”

Serikali yetu na isome alama za nyakati, ichukue hatua dhidi ya mafisadi.

Mkutno wa leo umefungua ukurasa mpya wa mapambano dhidi ya ufisadi. Mapambano haya hayana budi kuendelezwa na wananchi wote, wabunge wote, pamoja na wale wa CCM na viongozi wote.

Palipo na mafisadi hakuna maendeleo.

Penye nia pana njia.

Mungu ibariki Tanzania

Mungu tuepushea na mafisadi

Thursday, August 16, 2007

ZITTO KABWE ASIMAMISHWA UBUNGE!

Kama kuna mbunge ambaye anastahili ‘tuzo’ kwa kuiitenda kazi yake ipasavyo, nionavyo mimi mbunge huyo alipaswa kuwa ni Zitto Kabwe. Zitto ameonyesha kuwa shujaa na mwanamapinduzi anayetazamia kuiona Tanzania mpya kwa kujaribu kuitumia nafasi yake ya ubunge kuuondoa uozo ndani ya utawala uliopo!

Hapa ndipo ninapotamani kuanzishwa kwa tuzo hii, yawezekana isiwe ni pesa, kama ile zawadi inayotolewa na mfanya biashara maarufu, mwana wa Afrika,raia wa Sudan, Mo Ibrahim, ambaye amehaidi kuitoa kwa kiongozi atakaye kuwa muadilifu barani Afrika.

Tunaweza kufanya hivyo kwa wabunge watumishi wa watu, kama Zitto Kabwe ili kuwapa moyo kuendelea kupambana na mafisadi.Tuzo hii iwe ni ishara tu ya kuuthamini mchango wa mbunge husika ili ajue usahihi wa hoja anazozisimamia na nguvu ya umma iliyo nyuma yake.Nguvu ya mwanasiasa yoyote ni watu.

Iko wapi haki?,

Iko wapi demokrasi?,

Yako wapi maslahi ya taifa wanayoyalinda wabunge wetu?, mbona wamemtosa mpiganaji hodari aliyehitajika sana nasi wenye nchi?

Mbona Zitto kahukumiwa kukaa nje ya bunge hadi januari mwakani huku akiwa analitetea taifa lake linufaike na madini yake?

Je kuna tatizo gani kuchunguza mkataba uliosainiwa na waziri Karamagi katika mazingira ya utata tena ukasiniwa huko London na si hapa Tanzania?

Hili ni bunge la aina yake!

Yaani pale ndani we unga mkono tu!

Gongo gonga yale ma meza mara waziri akiwa anaongea kuashiria unakubaliana naye!

Kuna wakati Freeman Mbowe alilifananisha bunge letu na mchezo wa kuigiza!, mbunge wa chama kinachotawala hata kama amepinga hoja kwa manneno yake akimaliza kuongea anaiunga mkono kwa asilimia mia!

Swala aliloibua Zitto lilikuwa ni la msingi, wabunge wetu hawakuuona umsingi wake, wameangalia maslahi ya chama chao na matumbo yao na wakamtosa shujaa na mtetezi wetu ili kulinda maslahi yao na chama chao!

Hii ndio Tanzania yetu!

Hatuna budi kuipanga upya!

Hapa ilipo ni shaghalabagala!

Natamani Mwalimu Nyerere angalikuwa hai ayaone haya yanayotendeka ndani ya ardhi ya taifa aliloliasisi, najua asingalijizuia kuyakemea, potelea mbali hata kama wasingalimsikia. Kwa kuwa Mwalimu hayupo na tuwaambie hawa wabunge wa CCM mwendo huu wa kuwanyamazisha mashujaa na watetezi wetu siyo wenyewe!

Wapo wanaharakati walioanza kulisema hili.

Kuendelea na kautaratibu ka hovyo kama haka ka kuwasimamisha ubunge wabunge wenye hoja za msingi, kwa kisingizio chochote kile, ni kujenga bunge la wabunge waoga na kuendeleza taifa la mazuzu.

Ni kutowatendea haki watanzania.

Aluta kontinua!

Friday, August 10, 2007

ITAKUWAJE 2025?

Jiji la Dar es salaam linakuwa kwa kasi.

Cha ajabu ni kwamba mambo mengi yamebaki vile vile, yanayooongezeka hayaoani na idadi ya wakazi weanaozidi kuongezeka jijini kila kukicha. Kasi ya kuleta maendeleo yanayokidhi idadi ya watu ni ya mwendo wa konokono.

Bila kuendeleza vijiji, kupeleka huduma bora za kijamii kama elimu,afya,mabenki,umeme,watu wataendelea kukimbilia mijini!

Jiji limejaa,najiuliza ni lini wakuu wetu watahamia Dodoma kule wanakotuambia ndio mji mkuu wa nchi yetu, kila mmoja anataka kukaa Dar, viongozi nao hawataki kuhamia Dodoma.Wasomi wetu nao wanajazana Dar.Kuna nini Dar kisichowezekana kwingine?,Nani atakeayepeleka maendeleo hizo sehemu nyingine ikiwa kila mmoja asema “tutabanana hapa hapa”?, wabunge nao wakaa jijini, majimboni kwao wanakaa lini?,kaaazi kweli kweli!

Labda kuhama kwa wakuu na idara zao kutapunguza msongamano barabarani.

Asubuhi na jioni usafiri ni vurugu tupu. Wakuu hawaelewi taabu hii inayompata binadamu, raia na mkazi wa jiji hili Dar es salaam.Kama wanaelewa haliwakeri.Angalia watu wanavyopanda kwenye mabasi kupitia madirishani,angalia taabu anayoipata mwanafunzi ndani ya jiji hili.

Ndio maana natamani ndugu Lowasa akakae Mbagala japo kwa wiki moja, apande daladala kama sisi, aone taabu ya usafiri inavyomlazimisha kijana mtanashati kuuacha mlango na kuingilia dirishani, mradi tu aweze kuwahi kazini. Juzi kijana mmoja amefariki, akiwa anagombea daladala akaanguka ,gari ikamkanyaga,mauti ikamfika.

Ndio maana natamani ndugu Kandoro akakae Kigamboni japo kwa wiki moja tu aione taabu inayomkabili mtanzania anayetumia kivuko kibovu pasipo uhakika wa usalama wa maisha yake.

Ndio maana natamani mama Magret Sitta ahamie Gongo la Mboto japo kwa wiki moja ili aone jinsi wanafunzi wanavyopata taabu kupata usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.

Jiji limejaa, endapo hali ikiendelea hivi ilivyo, je 2025 itakuwaje?, patakuwa hapatoshi!

Tutafakari!