Friday, August 10, 2007

ITAKUWAJE 2025?

Jiji la Dar es salaam linakuwa kwa kasi.

Cha ajabu ni kwamba mambo mengi yamebaki vile vile, yanayooongezeka hayaoani na idadi ya wakazi weanaozidi kuongezeka jijini kila kukicha. Kasi ya kuleta maendeleo yanayokidhi idadi ya watu ni ya mwendo wa konokono.

Bila kuendeleza vijiji, kupeleka huduma bora za kijamii kama elimu,afya,mabenki,umeme,watu wataendelea kukimbilia mijini!

Jiji limejaa,najiuliza ni lini wakuu wetu watahamia Dodoma kule wanakotuambia ndio mji mkuu wa nchi yetu, kila mmoja anataka kukaa Dar, viongozi nao hawataki kuhamia Dodoma.Wasomi wetu nao wanajazana Dar.Kuna nini Dar kisichowezekana kwingine?,Nani atakeayepeleka maendeleo hizo sehemu nyingine ikiwa kila mmoja asema “tutabanana hapa hapa”?, wabunge nao wakaa jijini, majimboni kwao wanakaa lini?,kaaazi kweli kweli!

Labda kuhama kwa wakuu na idara zao kutapunguza msongamano barabarani.

Asubuhi na jioni usafiri ni vurugu tupu. Wakuu hawaelewi taabu hii inayompata binadamu, raia na mkazi wa jiji hili Dar es salaam.Kama wanaelewa haliwakeri.Angalia watu wanavyopanda kwenye mabasi kupitia madirishani,angalia taabu anayoipata mwanafunzi ndani ya jiji hili.

Ndio maana natamani ndugu Lowasa akakae Mbagala japo kwa wiki moja, apande daladala kama sisi, aone taabu ya usafiri inavyomlazimisha kijana mtanashati kuuacha mlango na kuingilia dirishani, mradi tu aweze kuwahi kazini. Juzi kijana mmoja amefariki, akiwa anagombea daladala akaanguka ,gari ikamkanyaga,mauti ikamfika.

Ndio maana natamani ndugu Kandoro akakae Kigamboni japo kwa wiki moja tu aione taabu inayomkabili mtanzania anayetumia kivuko kibovu pasipo uhakika wa usalama wa maisha yake.

Ndio maana natamani mama Magret Sitta ahamie Gongo la Mboto japo kwa wiki moja ili aone jinsi wanafunzi wanavyopata taabu kupata usafiri wa kwenda na kurudi shuleni.

Jiji limejaa, endapo hali ikiendelea hivi ilivyo, je 2025 itakuwaje?, patakuwa hapatoshi!

Tutafakari!

No comments: