Kama kuna mbunge ambaye anastahili ‘tuzo’ kwa kuiitenda kazi yake ipasavyo, nionavyo mimi mbunge huyo alipaswa kuwa ni Zitto Kabwe. Zitto ameonyesha kuwa shujaa na mwanamapinduzi anayetazamia kuiona Tanzania mpya kwa kujaribu kuitumia nafasi yake ya ubunge kuuondoa uozo ndani ya utawala uliopo!
Hapa ndipo ninapotamani kuanzishwa kwa tuzo hii, yawezekana isiwe ni pesa, kama ile zawadi inayotolewa na mfanya biashara maarufu, mwana wa Afrika,raia wa Sudan, Mo Ibrahim, ambaye amehaidi kuitoa kwa kiongozi atakaye kuwa muadilifu barani Afrika.
Tunaweza kufanya hivyo kwa wabunge watumishi wa watu, kama Zitto Kabwe ili kuwapa moyo kuendelea kupambana na mafisadi.Tuzo hii iwe ni ishara tu ya kuuthamini mchango wa mbunge husika ili ajue usahihi wa hoja anazozisimamia na nguvu ya umma iliyo nyuma yake.Nguvu ya mwanasiasa yoyote ni watu.
Iko wapi haki?,
Iko wapi demokrasi?,
Yako wapi maslahi ya taifa wanayoyalinda wabunge wetu?, mbona wamemtosa mpiganaji hodari aliyehitajika sana nasi wenye nchi?
Mbona Zitto kahukumiwa kukaa nje ya bunge hadi januari mwakani huku akiwa analitetea taifa lake linufaike na madini yake?
Je kuna tatizo gani kuchunguza mkataba uliosainiwa na waziri Karamagi katika mazingira ya utata tena ukasiniwa huko London na si hapa Tanzania?
Hili ni bunge la aina yake!
Yaani pale ndani we unga mkono tu!
Gongo gonga yale ma meza mara waziri akiwa anaongea kuashiria unakubaliana naye!
Kuna wakati Freeman Mbowe alilifananisha bunge letu na mchezo wa kuigiza!, mbunge wa chama kinachotawala hata kama amepinga hoja kwa manneno yake akimaliza kuongea anaiunga mkono kwa asilimia mia!
Swala aliloibua Zitto lilikuwa ni la msingi, wabunge wetu hawakuuona umsingi wake, wameangalia maslahi ya chama chao na matumbo yao na wakamtosa shujaa na mtetezi wetu ili kulinda maslahi yao na chama chao!
Hii ndio Tanzania yetu!
Hatuna budi kuipanga upya!
Hapa ilipo ni shaghalabagala!
Natamani Mwalimu Nyerere angalikuwa hai ayaone haya yanayotendeka ndani ya ardhi ya taifa aliloliasisi, najua asingalijizuia kuyakemea, potelea mbali hata kama wasingalimsikia. Kwa kuwa Mwalimu hayupo na tuwaambie hawa wabunge wa CCM mwendo huu wa kuwanyamazisha mashujaa na watetezi wetu siyo wenyewe!
Wapo wanaharakati walioanza kulisema hili.
Kuendelea na kautaratibu ka hovyo kama haka ka kuwasimamisha ubunge wabunge wenye hoja za msingi, kwa kisingizio chochote kile, ni kujenga bunge la wabunge waoga na kuendeleza taifa la mazuzu.
Ni kutowatendea haki watanzania.
Aluta kontinua!
1 comment:
Bwana Pius,
Pole sana kwa kumlilia Zitto. Nimesoma habari zake kwenye mtandao, kama ni kweli yaliyoelezwa ndivyo yalivyokuwa Bungeni, Basi Taifa linakoelekea ni kubaya. inawezekana Bunge linataka mtu anayetumia soft language kwa mfano badala ya kusema Waziri ni Muongo, basi Zitto angetumia neno "alikosea" pengine lingepunguza Hasira za waziri Karamagi. But Watanzania tunasahau kitu kimoja, kwamba Karamagi ni mfanyabiashara sasa ukimpa nafasi mfanyabiashara unategemea nini? Mwalimu aliwahi kukemea wafanyabiashara kuwa na mazoea na Ikulu, Yesu Kristo tunaambiwa aliwahi kuwafukuza wafanyabiashara hekaluni. hawa wote walikuwa wanajua madhara ya wafanyabiashara, hawatosheki hata kama bakuli limejaa. Leo sisi tunawapa nafasi nyeti bila kuchunguza utajiri wao waliupataje. ukifanya uchunguzi utagundua kwamba ni asilimia kumi tu ya wafanyabiashara walioko TZ ndio pengine utajiri wao ni halali. Waziri Karamagi inawezekana yuko katika kundi la wengi, lazima afanye kila njia ili asichunguzwe. Hapo imetumika hoja ya nguvu badala ya nguvu ya hoja. Tuendelee kuwaunga mkono wale wote wanaotetea maslahi ya taifa letu. tuendelee kuanika uozo wowote kwa njia za mtandao. hata lile sakata la BOT linatakiwa kuendelea kuandikwa tena lipostiwe kwenye vyombo vya kimataifa ili watu wengi pamoja na wafadhili wayasome. pengine hiyo itasaidia kulazimisha serikali zetu badhilifu kuchukua hatua.
Mwisho nawapongeza wote wanaofichua uozo wa viongozi wetu bila woga.
Mike.
Post a Comment