Sunday, October 14, 2007

NYERERE DAY

Ninaikumbuka siku hii ya leo, miaka 8 iliyopita, tarehe 14 october 1999,nikiwa mwaka wa kwanza katika chuo kikuu cha Dar es salaam, kitivo cha uhandisi, nakumbuka tulikwa kwenye kipindi katika karakana ya umeme. Mara tukasikia wimbo wa taifa unapigwa,kila mmoja anaikimbilia radio kisha tunamsikia raisi wa awamu ya tatu,Mkapa anatangaza Mwalimu Nyerere amefariki dunia! Baada ya muda uongozi wa chuo unatoa tangazo la kusimamisha ratiba zote za vipindi.Ilikuwa mshtuko mkubwa.Baada ya siku kadhaa mwili unawasili Tanzania chuo kikapanga utaratibu mzuri wa kuwawezesha wanachuo kwenda kuuaga mwili wa hayati Mwalimu Nyerere,nilikuwa mmoja wa waliofika uwanja wa taifa kuuaga mwili wa Mwalimu, usiku wa manane lakini ilikuwa kama mchana jinsi watu walivyojaa.Umati ule unanifundisha jambo moja 'kuongoza ni kujitoa kwa ajili ya unaowaongoza', Mwalimu aliyatoa maisha yake kwa ajili ya taifa lake, aliishi alichokisema na alisema alichokiishi tofauti na viongozi wetu wa leo!

Tunapoikumbuka siku ya kufariki kwa Mwalimu Nyerere hii leo tujiulize maswali yafuatayo:-

Hivi mwalimu angalikuwepo soo kama la Richmond Development Cooperation lingepita kimizengwe vile na mambo yakaisha kiaina kama yalivyoisha?
Sasa tunaambiwa kuwa mkataba ule ulisainiwa usiku na Tanesco hawajui ni nani aliyeusaini. Inashangaza!

Hivi ule mkataba tata wa madini wa Buzwagi ungepita hivihivi bila kuundiwa tume huru aliyoiomba Mbunge Zitto?
Bila shaka Mwalimu angemwagia sifa Zitto Kabwe hadharani na kuwasuta wabunge wa CCM waliomfukuza bungeni.Bila shaka angesema kuna haja ya waziri Karamagi ajiuzulu!

Hivi ile kashfa ya ufisadi aliyoiibua Dk Slaa, wale waliotajwa angelipuuziwa kama ambavyo wanafunzi wake wamepuuzia? Bila shaka angaliwaita wote Butiama na kuwahoji maswali magumu, na labda angalishauri baadhi yao wajiuzulu!

Hivi Mwalimu angalikuwepo wanafunzi Mlimani wangelipishwa 40% ya ada? Bila shaka angalikemea kwa nguvu zote!

Huyu ndiye Mwalimi ambaye miaka nane sasa bila yeye viongozi wetu wameshindwa kuweka dhamira yao kwa dhati na kwa vitendo kupambana na ufisadi, kwani hata ndani ya chanma alichokiasisi yeye Mwalimu nguvu ya pesa inatumika kupata uongozi!

Miaka minane bila Mwalimu Nyerere ujumbe kwa viongozi wetu ni kuwa, wamuenzi Mwalimu kwa vitendo na si kwa maneno kama wafanyavyo sasa,tumechoshwa na porojo, tumeschoshwa na maneno tunataka vitendo.

2 comments:

Simon Kitururu said...

Kweli tutamkumbuka Mwalimu.

Pius Ntwale said...

Ni kweli Simon, tena tutamkumbuka vizazi na vizazi,ila kumkumbuka tu haitoshi, tunaishi vipi kwenye misingi ya maadili aliyotuachia?, je watoto wetu ni maadili gani ya kiuongozi wanayoyaona kwa viongozi wetu wa sasa?, ndio maana kuna waungwana wanasema kama Mwalimu atafufuka leo,atakufa tena kwa pressure kwa jinsi nchi inavyoendelea kwa kuelekea kushoto na kuuacha muelekeo sahihi wa kuelekea kulia aliotufundisha Mwalimu.