Wednesday, October 24, 2007

GAZETI JIPYA RAIA MWEMA!

Moja ya magazeti ambayo nilitokea kuyapenda kwa muda mrefu sana ni gazeti la Rai.Hii ilitokana na umakini na ujasiri wa waandishi wa gazeti hili.Ninaamini kabisa kuwa magazeti yana sehemu kubwa katika kujenga fikra zetu, kutufundisha, kutuelimisha, kutuburudisha na kutuonyesha uozo, au tuuite ufisadi, ndani ya jamii yetu na hata namna ya kupambana na uozo huo. Magazeti yakiandika habari za kweli na kwa uwazi yataweza kuisaidia jamii yetu kusonga mbele kifikra na kimaendeleo.

Nakiri kwa kusema kuwa hamu ya kulisoma gazeti la Rai imenitoka,siku hizi nalinunua kwa mazoea tu, umakini na uandishi wa gazeti hili sio ule wa walipokuwa wakiandika akina Jenerali Ulimwengu na Maggid Mjengwa.Nadhani sasa gazeti hili jipya la “Raia Mwema” litaziba pengo lililoanza kujitokez andani ya Rai, sijui gazeti la Rai limekumbwa na nini.Sielewi!

Muda mfupi nimeisoma habari ya kuanzishwa kwa gazeti hili, na wiki ijayo inatoa toleo la kwanza, miongoni mwa waandishi ni Jenarali Ulimwengu, Prof Issa Shivji,Maggid Mjengwa, Mihangwa na Padri Pivatus Karugendo.Kama unawafahamu waandishi hawa basi usikose kusoma makala zao!.Utaniambia mwenyewe!

Sina shaka na hawa waandishi kuwa kuwa wamekubuhu katika taaluma ya uandishi wa habari, watakuwa na ujasiri wa uandika yale ambayo wengine wameogopa, watashiriki katika mchakato wa kuisafisha jamii yetu inayoendelea kuchafuliwa na ufisadi, utandawizi na mmong’onyoko wa maadili.

Kila la kheri gazeti la “RAIA MWEMA” ninaahidi kukunua kila utokapo!

No comments: