Monday, September 17, 2007

Dk SLAA NI MFANO WA KUIGWA AUNGWE MKONO NA WATANZANIA WOTE!

Jana nilikuwa na usongo kweli wa kujua siku ya jumamosi ni watu gani ambao Dr Slaa aliwataja kama alivyoahidi,yaani wale wanaohusika na ubadhirifu wa fedha ya umma, kama ilivyo ada kwangu kwa siku za jumapili ninaelekea kanisani, kichwani nimepanga nikitoka tu nilisake gazeti lenye majina hayo. Nashawishika kununua gazeti la mwananchi lenye kichwa cha habari "Dk Slaa ataja vigogo wanaoitafuna nchi".Nilidhani ntayakuta majina mle ndani niwajue mafisadi hawa, wadau wa umasikini wa mtanzania azungukwaye na utajiri wa kila aina.

Kwa mshangao mkubwa sioni jina hata moja, zaidi ya kuona hawa waandishi wetu wa habari wanaandika,"miongoni mwa waliotajwa na Dk Slaa ni makatibu wakuu, wabunge wawili na mawaziri".Yaani kiujumla tu namna hiyo, halafu ndo imetoka.Hivi waliogopa nini kusema majina, mimi sijui taratibu za waandishi kwani hiyo si taaluma yangu, lakini wao si wangemnukuu tu Dk Slaa alichosema, tangu lini mjumbe akauwawa?

Kama na wewe hukuridhishwa na habari za vyombo vyetu vya habari siku ile basi tupia jicho pale kwa Mzee Mwanakijiji, amerusha hotuba ile msikilize na umsome kwa kubonyeza hapa.

Waandishi wa habari ni wakati sasa muanze kuthubutu kuwataja watu kwa majina jamii iwajue, hawa mafisadi ndio maadui wa uchumi wetu, hawa ndio maadui walioongezea wale kina ujinga, maradhi na umasikini, yaani amaadui hawa wametutengenezea adui aitwaye ufisadi au rushwa.Hawa wanapaswa kuchunguzwa na ikithibitika tuhuma zinazowakabili ni za kweli wafilisiwe na waukabili mkono wa sheria.

Hatuwezi kupiga hatua mbele kiuchumi kama tutaendelea kuwakumbatia hawa wezi, mafisadi wanaoitafuna nchi yetu,huku ndugu zetu wakikosa huduma bora za afya, elimu, maji safi, makazi bora nk

Tunataka kuona kuwa ile kauli mbiu ya maisha bora kwa kila mtanzania haikuwa danganya toto ya kupatia kula 'kura' bali ilikuwa na nia ya kweli ya kuboresha maisha ya mtanzania.

Takukuru nao wazifanyie kazi taarifa hizo, wawachunguize, kwani ni kazi yao.

Kitendo alichokifanya Dk Slaa ni cha kijasiri na cha kuungwa mkono na watanzania wote.

Tuamke sasa tupambane na maadui wa uchumi wetu.

No comments: