Friday, September 28, 2007

HOJA YA KUANZISHWA BLOGU YA WABUNGE NA WANANCHI!

Mara nyingi katika mijadala isiyo rasmi ninayoifanya na watu mbalimbali tunapojadili mambo ya siasa tunakubaliana kuwa tatizo kubwa la siasa ya nchini kwetu ni mfumo mzima unaoendesha siasa.Ni kama vile wananchi hatuna sauti na nguvu ya kuwaaambia wawakilishi wetu bungeni kuwa ni nini tunataka, na wao wakakisimamia kuhakikisha kinafanyika, kwa hali ilivyo sasa ni kama vile wabunge hatujawatuma wametumwa na chama hasa wale wa CCM.Wanasikiliza zaidi chama kuliko wananchi wanaowawakilisha.Mfumo huu haufai na tunaweza kuurekebisha.

Hivi kwa nini kusiwe na blogu, mfano www.wasiliananawabunge.blogspot.com, ambayo itawakutanisha wananchi na wabunge,kabla ya wabunge kwenda Dodoma na wakati wakiwa Dodoma tuwaeleze nini waihoji serikali kwa niaba yetu, na tusiporidhika wakiwa huko huko Dodoma tuwaeleze hatujaridhika na majibu ya Serikali ili wahoji, wahoji na wahoji hadi majibu yapatikane.Vinginevyo tutaendelea kusikia majibu ya porojo ya kila siku wanayojibu mawaziri wetu ,yasiyo na nguvu ya uwajibikaji, majibu kama, serikali iko mbioni kushughulikia swala x,serikali inafuatilia kwa karibu suala y,serikali ina mkakati wa kufanya swala z,serikali imejizatiti kuondoa uasikini ifikapo mwaka f,serikali inafanya kila linalowezekana kuhakikisha kero h inakwisha, majibu haya hayatoshi na yanahitaji maswali mengine zaidi lakini wabunge wetu huridhika nayo.

Wakati umefika sasa wa kuwa na jukwaa la kuwaambia wabunge wetu pale tunapotaka waihoji serikali na tusiporidhishwa na majibu ya serikali.

Blogu hii pia iwe na e mail address na namba za simu za wabunge wote.

Tutaendelea kuyanyoosha yaliyopinda, hadi pale yatakaponyooka.

Hoja hii ninaikabidhi jumuiya ya wanablogu Tanzania, JUMUWATA, ikifaa ifanyiwe kazi na isipofaa itupiliwe mbali.

Naomba kuwasilisha!

3 comments:

Simon Kitururu said...

Kazi bomba Mkuu!
Tuko Pamoja!

Egidio Ndabagoye said...

Kuna jamaa alinishtua kuwa hawa "wawakilishi" hata anuani za barua pepe hawana! na kwa wale wachache walizonazo kusoma hawasomi.
Endeleza libeneke

Pius Ntwale said...

Nakushukuru Simon,kwa kunitembelea!
sasa kumekucha mkuu.

Ndabagoye uyasemayo yaweza kabisa kuwa na ukweli,kwani mle ndani wamo walioanza katika uongozi na Mwalimu Nyerere hadi leo wapo,kama vile vijana wanaofaa hawapo,wanaendesha mambo kizamani na kimazoea tu! sishangai kusikia hawana muda hata wa kusoma e mail kwa wale walionazo na wasionazo kutoona umuhumu wa kuwa na e mail, really? in this world of science and technology? "eti wako bize"