Thursday, September 27, 2007

KISWAHILI NA KIINGEREZA KIPI ZAIDI?

Bila shaka usomapo unajibu la swali hapo juu?, najiuliza tu.Waafrika tuna kaugonjwa fulani kakudharau cha kwetu. Ndio.Yawezekana ni athari za ukoloni, waliviita vya kwetu vya kishenzi nasi tukaviona hivyo na kuvitukuza vya kwao na hii iko hadi leo.
Hii imepelekea kuiga kila cha mzungu, angalia leo utamaduni wetu ulivyopindapinda, haueleweki,sijui ni nini utambulisho wa mtanzania wa leo.Mimi nadhani ni Kiswahili chake tu!

Angalia dada zetu vivazi vyao, kuna wakati kulikuwa na uvumi kuwa presidenti wetu kapiga marufuku aina fulani ya vivazi vya dada zetu,wao wanaita vya kizungu,wengine waita vya kihuni!, jamaa wakazua kuwa mgambo watatanda na bakora halafu aonekane binti na kivazi cha kutatiza,analamba viboko kadhaa kama adhabu na onyo.Siku moja waandishi wa habari wakapata upenyo wakamuuliza mkuu, akajibu hana mpango wa kuchukua hatua hiyo, hayo ni mambo ya fashion tu, yatapita kama zilivyopita suruali za chini nimwagie miaka ileeeeeeeee. Vijana wa kiume wa kileo nao wamekuwa wazungu, wanasuka nywele, suruali zinavaliwa chini ya matako, ati mambo ya kizungu!.Mambo ya kuiga hayo!
Ni kwa vipi tutaweza kuulinda utamaduni wetu ulioingiliwa na utandawazi?

Leo hii tunaona kiingereza ni bora kuliko Kiswahili, tunaona hakifai kutumika kama lugha ya kufundishia, kama lugha inayofaa kutumika maofisini.Je tatizo hili ni la lugha au wenye lugha?.Si kuwa lugha ya kiswahili haiwezi kubeba kazi hizi, wenye lugha wameidharau lugha yao wamekitukuza kiingereza zaidi.Yawezekana kuwa lugha hii ina mapungufu lakini upungufu huu hauhalalishi kutokufaa kwa lugha hii, upungufu huu ni changamoto kwa wataalamu wetu wa kiswahili waweze kukiwezesha kiswahili kujitosheleza kutumika, mitaani kuwasiliana, mashuleni kufundishia, maofisini kwa mawasiliano ya kikazi.Wataalamu wetu watafsiri kwa kiswahili fasaha kila kilicho kwa kiingereza kiandikwe kwa kiswahili, kila kitu, vitabu vya mashuleni,maofisini,sheria zitumikazo mahakamani, vitabu vya maelekezo kwa wakulima juu ya matumizi ya mbolea na umwagiliaji,mikataba yote nchi hii inayoingia itafsiriwe pia ili wale wasio ijua lugha ya kiingereza waelewe yaliyoandikwa.

Kuna mwalimu wangu mmoja alinifundisha hesabu, tuition, enzi hizoooooooooooo, alijulikana kwa jina la ‘Mr So Much’, anasagia kwelikweli kiswahili anasema hakifai, anatupa mfano, anasema, kama kiswahili kingetumika kufundishia ingekuwa taaaabu kwelikweli, anatoa mfano, hapo anafundisha topic ya calculus, differentiation, sentensi kama ‘we differentiate y with respect to x’,dy/dx, tungesema ‘tunanyambulisha x kwa heshima ya y’, hapo hoja yake inakuwa kiswahili hakitoshi kufundishia na anatushawishi.Kwa wakati ule alitushawishi wengi tukakubali kuwa kiswahili hakifai kufundishia.Nadhani kina mapungufu yanayohitaji kurekebishwa na kuboreshwa.

Ukweli ulio wazi ni kwamba kiingereza ni kikwazo kikubwa kwa wanafunzi kuelewa masomo yao darasani na kufaulu usahili wanapoomba ajira.Endapo Kiswahili kitatumika kama lugha ya kufundishia kitamuwezesha mwanafunzi kuyapokea maarifa anayopewa na mwalimu wake kwa urahisi zaidi, ilivyo sasa mwanafunzi inabidi amsikilize mwalimu, atafsiri kinachofundishwa kutoka kiingereza kwenda kiswahili,akifanyie kazi akilini na kukihifadhi kwenye ubongo.Akishindwa kutafsiri alichosikia atashindwa kuelewa pia, hata kama atakiweka kwenye ubongo atakuwa amekariri tu na hili ndio tatizo tulilonalo hapa Tanzania.Ndio maana elimu yetu ni bora lakini haitoi maarifa ya kutosha kutuwezesha kupiga hatua mbele kiuchumi,kiteknolojia na kijamii.

Kama kiingereza kinaweza, kiswahili pia kinaweza, ingawa safari ya kukiwezesha ni ndefu na si rahisi!

No comments: